Na Hendrick Msangi:
Kamati ya Bunge inayosimamia mambo ya afya na maswala ya Ukimwi, Machi 15, 2024 imefanya ziara Kata ya Bugulula Halmashauri ya Wilaya ya Geita ili kuzungumza na wanafunzi pamoja na kuona namna ambavyo wanafunzi hao wamejifunza jinsi ya kupambana na kudhibiti ugonjwa hatari wa Ukimwi.
Awali akisoma taarifa mbele ya Kamati ya kudumu ya Bunge inayosimamia sekta ya afya na maswala ya Ukimwi, Mkurengezi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita ndugu Karia Rajabu Magaro amesema jitihada zinafanyika kukabiliana na janga la Ukimwi ambapo jumla ya vituo 53 vya tiba vinatoa huduma rafiki kwa vijana.
Aidha Magaro amesema Halmashauri inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuendeleza juhudi za kuwajengea uwezo wananchi kutambua athari zitokanazo na Ukimwi ikiwa ni pamoja na kuwa tayari kujitokeza kupima, na kuwahimiza kutumia dawa wale ambao wamekutwa na maambukizi ya VVU.
Pamoja na hayo Mkuregenzi Magaro ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita kwa kuendelea kutoa fedha, kuweka mazingira wezeshi na kujenga uwezo wa wahusika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo huku akiutaja Mradi wa Timiza Malengo ambao umetoa mitaji ya kuanzisha biashara ambapo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Geita julma ya Kata 37 na vijiji 145 zimenufaika na mradi huo ambapo shilingi 146,575,700 zilipokelewa huku jumla ya mabinti 571 wakinufaika kila mmoja kiasi cha shilingi 256,700 kama mtaji wa biashara.
Wajasiriamali kata ya Bugulula ambao ni wanufaika wa mradi wa Timiza Malengo wakiileza kamati ya Bunge inayosimamia sekta ya afya na maswala ya Ukimwi mafanikio waliyoyapata baada ya kuwezeshwa kiasi cha shilingi 250,000 kila mmoja ambapo wamesema kupitia mtaji huo wameweza kuwasomesha watoto, kujenga na kuzihudumia familia zao.
Mradi wa Timiza Malengo ulianza kutekelezwa na serikali katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita 2022/2023 pamoja na mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali ya AMREF Tanzania pamoja na TAYOA, Ukiratibiwa na ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Tume ya Kudhibiti UKIMWI-TACAIDS kwa ufadhili wa mfuko wa Dunia (Global Fund) ambao lengo lake ni kuwasaidia wasiachana balehe, na wanawake vijana wenye umri wa miaka 10 hadi 24 walioko shuleni kuhitimu elimu na walio nje ya mfumo wa elimu kuwezeshwa kijamii na kiuchumi ili kujikimu kimaisha wakiwa salama dhidi ya VVU na UKIMWI.
Naye Mwenyekiti wa kamati ya Bunge inayosimamia mambo ya afya na maswala ya Ukimwi, Mhe Stanslaus Haroon Nyongo ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki amewataka wanafunzi wa shule ya msingi Bugulula kutokujamiana ili kuepuka kupata maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi pamoja na magonjwa mengine yanayotokana na ngono zembe pamoja na mimba za utotoni na kuwataka kutoa taarifa kwa walimu au wazazi wao pale wanapoona kuna watu wanawasumbua ikiwa ni pamoja kuwashauri wazazi wao kuwahimiza kutumia dawa wale ambao wamepata maambukizi na kuepuka unyanyapaa kwa wagonjwa wenye maambukizi ya VVU.
Waheshimiwa wabunge kamati ya bunge inayosimamia sekta ya afya na maswala ya ukimwi walipotembelea shule ya Msingi Bugulula kata ya Bugulula iliyoko Halmashauri ya Wilaya ya Geita
“Tumetembelea maeneo mbalimbali kujionea uwekezaji mkubwa unaofanywa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika sekta ya afya na leo tupo Geita Kata ya Bugulula, Mhe Rais anatutaka watanzania wote tuwe na afya bora ndio maana amewekeza kwenye vituo vya afya, kwenye zahanati, hospitali za wilaya,hospitali za Mikoa, Kanda na Hospitali za Rufa, tumepita kuona ni jinsi gani serikali imefanya kazi kubwa katika kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi” Alisema Mhe Nyongo.
Kwa upande wake Mhe Ummy Nderiananga Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu amewataka wanafunzi hao kuendelea kuweka bidii katika masomo yao na kutokuwanyanyapaa waathirika wa maambukizi ya VVU.
Mhe Ummy Nderiananga Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu akizungumza na wanafunzi wa shule ya msingi Bugulula ambapo amewata kuepuka unyanyapaa kwa waathirika VVU.
Wakiendelea kuwahusia wanafunzi wa shule ya msingi Bugulula, Mbunge wa jimbo la Mtambwe kaskazini Pemba Mhe Khalifa Mohamed Issa amewata wanafunzi hao kusoma kwa bidii ili wafanikiwe huku wakilishika somo la Ukimwi kwani Ukimwi bado upo na unaua na kuwataka kuacha unyanyapaa kwa wale ambao wamegundulika kuwa na maambukizi ya virusi vya ukimwi ikiwa ni pamoja na kutumia dawa kama wanavyoelekezwa na madaktari.
Kamati hiyo ya Bunge imepita katika shule hiyo ya msingi ya Bugulula kujionea jinsi wanafunzi hao walivyojifunza mbinu mbalimbali za namna ya kupambana ukimwi na ikiwa ni pamoja na kupunguza unyanyapaa.
Pamoja na kutembelea shule ya msingi Bugulula, kamati hiyo iliwetembelea wajasiriamali kata ya Bugulula ambao ni wanufanika wa Mradi wa Timiza Malengo ambao umewawezesha kujikwamua kiuchumi ili kuepuka kufanya kazi ambazo zinaweza kuwa hatarishi na kupelekea kupata maambukizi ya Ukimwi. “Endeleeni kufanya biashara ili msiingie kwenye mazingira hatarishi na kusababisha kupata maambukizi ya vvu” alisema Mhe Nyongo.
Naye Mhe Diwani wa kata ya Bugulula Mhe Lupuga aliishukuru Kamati hiyo na kuiomba kuendelea kuweka nguvu ili kituo cha afya cha Kasota kianze kutoa huduma ya upasuaji kwani kituo hicho kimekamilika vifaa vyote isipokuwa huduma ya upasuaji wa dharura ambapo Halmashauri kupitia ofisi ya Mkuregenzi ilisema bajeti ya ukamilishwaji inaendelea na ifikapo mwezi wanne kituo hicho kitaanza kutoa huduma ya upasuaji.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mhe Charles Kazungu akiishukuru kamati ya Bunge kwa kuitembelea Halmashauri ya Wilaya ya Geita Machi 15,2024 ambapo amesema Wilaya ya Geita itaendelea kuiunga mkono serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Kwa niaba ya baraza la madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mhe Charles Kazungu ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kuleta fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi katika miradi ya shule na huduma za afya pamoja na kamati hiyo ya Bunge kwa kuitembelea Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa