Wito umetolewa kwa jamii kubadilisha tabia,sambamba na wazazi kufuatilia mienendo ya watoto wao, ili kudhibiti maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI kwa vijana walio na umri chini ya miaka 25, kwa kuwa UKIMWI bado upo.
Hayo yamebainishwa na Mratibu wa Mwitikio wa kupambana na UKIMWI,wa Halmashauri ya wilaya ya Geita Bi.Patricia Laurent Nsinde,ambapo amesema kuwa matokeo ya kitaifa ya utafiti wa mwaka 2017/2018, yanaonyesha kuwa maambukizi mapya kwa vijana wenye umri kati ya miaka 15-24 ni 40%, huku mabinti wakiwa ni 80% katika hizo 40%.
Bi.Patricia amesema kuwa jamii haipaswi kuupuuzia ugonjwa huo, badala yake inatakiwa kuchukua tahadhari zote za kujikinga, huku akiwakumbusha wazazi kufuatilia mienendo ya watoto wao, ili kuwaepusha na tabia zote hatarishi ikiwemo kushiriki ngono zembe.
Amesema kuwa katika kuwasaidia vijana wa umri huo,Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imechukua hatua kadhaa, kama vile kutoa elimu kwa makundi yaliyo katika mazingira hatarishi, kama wahudumu wa baa,nyumba za kulala wageni,sehemu za migodini na maeneo ya uvuvi,sambamba na kuundwa kwa vilabu vya UKIMWI katika shule 30 za sekondari kwa lengo la kuendelea kuwaelimisha vijana.
Aidha Bi.Patricia amesisitiza kuwa ingawa elimu inatolewa, lakini jamii inapaswa kubadili tabia kwa kurekebisha baadhi ya mifumo hatarishi kwa kuwalinda mabinti na wanawake vijana hata kama hawasomi,sambamba na kupinga ajira zenye malipo madogo, hali inayowashawishi baadhi ya mabinti kufanya kazi hatarishi ili kukidhi mahitaji yao.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa