Na: Hendrick Msangi
MAADHIMISHO ya siku ya Afya na Lishe na Uzinduzi wa chanjo Kiwilaya yamefanyika Aprili 4, 2024 katika kata ya Lwezera na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama, serikali na taasisi za dini pamoja na kuambatana na burudani ya ngoma za asili na nyimbo za burudani.
Akizungumza katika maadhimisho hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Bi Bless Mwakyusa ambaye ni Mkuu wa Idara ya Utawala na rasilimiali watu Halmashauri ya wilaya ya Geita amewasihi wananchi kuhakikisha maswala ya Lishe ya watoto yanapewa kipaumbele kuanzia majumbani kwenye ngazi ya kaya hadi shuleni.
Mhe Chinchina ambaye ni Diwani wa Kata ya Lwezera akiwa na Maafisa na wadau mbalimbali pamoja na Watoto waliojitokeza kwenye siku ya maadhimisho ya siku ya afya na lishe na uzinduzi wa chanjo wakinywa uji wenye virutubisho ambao uliandaliwa na wazazi waliopewa semina elekezi ya namna ya kuandaa uji huo katika maadhimisho ya sikuya afya na lishe na uzinduzi wa chanjo
Akiendelea kuzungumza katika ufunguzi wa maadhimisho hayo, Bi Bless amewataka watumishi wote wa idara ya afya na Lishe kuendelea kutoa ushirikiano kwa jamii katika maswala ya lishe.
“Mkashirikiane na Idara mtambuka, wadau wa maendeleo na wananchi wote kwa ujumla kuhakikisha maswala ya lishe yanapewa kipaumbele kwani lishe ni suala mtambuka linalohusisha wadau wote na wananchi hasa katika muktadha mzima wa kubadili tabia ya ulaji wa vyakula unaozingatia misingi ya lishe.”alisema Bi Bless Mwakyusa.
Wananchi wakisikiliza hotuba ya Mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Idara ya Utawala na Rasilimali watu Bi Bless Mwakyusa wakati wa maadhimisho ya siku ya afya na lishena uzinduzi wa chanjo.
Pamoja na hayo bi Bless amesema Lishe duni hupelekea kuhatarisha ufaulu wa watoto wanapofikia umri wa kwenda shule, pamoja na kuathiri ustawi wa kimwili na utendaji wa kiaikili kwa watoto ikiwa ni pamoja na kuleta athari katika afya ya uzazi mambo ambayo hutokana na uelewa hafifu juu ya ulishaji wa vyakula sahihi kwa watoto na ambao hauzingatii makundi 6 ya chakula.
Bi Bless amewataka wazazi na walezi kuweka mikakati itakayoweza kuboresha lishe kwa watoto ikiwa ni pamoja na kuwanyonyesha watoto kwa kipindi cha miezi 6 na pindi watakapo maliza miezi 6 walishwe chakula mchanganyiko.
Afisa Utumishi huyo amewasihi wazazi kuwapa watoto mlo kamili na salama na kuwataka kuadhimisha siku ya afya na lishe kwa kila kijiji kila robo ya mwaka pamoja na kutoa elimu ya afua za lishe ili kuendelea kukabiliana na utapiamlo na udumavu ndani ya jamii na kuhakikisha inakuwa salama na yenye afya bora
Naye Afisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Bi Nasim Ginga amesema lengo la maadhimisho hayo ni kuendelea kuongeza hamasa, kujenga uwezo wa pamoja na kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu faida za lishe bora na madhara ya lishe duni katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Afisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Bi Nasim Ginga akimuelezea Mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Idara ya Utawala na Rasilimali watu aina ya vyakula ambayo vinatumika kuandaa lishe bora kwa watoto.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Lwezera ambapo maadhimisho hayo yamefanyika Mhe Chinchina ametoa wito kwa wananchi wa kata hiyo kuendelea kuyatumia maeneo wanayoishi kwa ajili ya kilimo ili kuendelea kupata lishe na kuomba uongozi wa Halmashauri kusogeza huduma za vipimo vya lishe kuepuka kwenda mbali kuvifuata ili kuendelea kuhamasisha wananchi.
Akifunga maadhimisho hayo Bi Bless amesema Serikali inayoongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuendelea kutoa elimu na hamasa ya afua za lishe kuanzia kwenye shule na jamii kwa ujumla.
Hata hivyo Bi Bless alizitaka kila shule kuhakikisha zinakuwa na viwanja vya michezo kwa ajili ya wanafunzi, kutenga maeneo kwa ajili ya bustani za mbogamboga, miche ya matunda na ufugaji wa wanyama wadogo ili kuendelea kupunguza athari zitokano na lishe duni kwani kwa mujibu wa tafiti zilizofanyika imebainika Mkoa wa Geita kuwa na idadi kubwa ya watoto walio duma kwa asilimia 38.6.
Maadhimisho hayo yamekuwa na manufaa makubwa kwa washiriki na wadau waliohudhuria ambapo wamejifunza namna ya kuandaa uji bora wa lishe kwa ajili ya watoto pamoja na kuwafahamu wadau na maafisa wanaosimamia masuala ya afya na lishe.
Msimamizi wa huduma za afya ngazi ya jamii Halmashauri ya Wilaya ya Geita Bi Amida Yindi akiwasajili watoto kwenye daftari la Mradi wa Lishe USAID Afya Yangu (RMNCAH). Pamoja na usajili huo wazazi hao walisisitizwa kupatia vyakula vya lishe ikiwa ni pamoja na kuwanyonyesha watoto ambao hawajafikia umri wa kupewa vyakula vya nyongeza.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita inaendelea kuishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya sekta ya afya pamoja na kuendelea kuratibu na kusimamia sera zinazohusu masuala ya lishe kama hatua ya kukabiliana na utapiamlo na udumavu ndani ya jamii na kuhakikisha inakuwa salama na yenye afya bora na ustawi ambayo itachangia kikamilifu katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Maafisa Lishe wakiwa katika zoezi la kuwapima watoto katika maadhimisho ya siku ya afya na lishe na uzinduzi wa chanjo yenye kaulimbiu isemayo Lishe Bora ni Msingi wa Maendeleo, SoteTuwajibike.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa