Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mhe. Hashim Komba, amesema kuwa ni muhimu kwa Halmashauri kuja na njia mbadala lakini sahihi kwenye shughuli za ukusanyaji wa mapato ili kuongeza mapato kwenye Halmashauri husika pamoja na kufikia malengo ambayo Halmashauri imeweka.
Akizungumza Julai 11 2025, katika ukumbi wa EPZ-Bombambili Manispaa ya Geita kwenye Kikao Kazi cha kujadili tathmini ya mwaka wa fedha 2024/2025 kwa Wakuu wa Idara na Vitengo kutoka Halmashauri ya Wilaya pamoja na wa Halmashauri ya Manispaa, Geita, Mhe. Komba ametoa pongezi kwa Wakurugenzi wa Halmashauri hizo kwa kusimamia maelekezo ya Serikali kwenye suala la ukusanyaji wa mapato, uliowezesha uvukaji wa bajeti ulokasimiwa kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Aidha, Mhe. Komba amesema kuwa, Halmashauri hizo zinapaswa kuongeza ubunifu kwa kujielekeza kwenye miradi mikubwa na ya kimkakati badala ya kutegemea sekta ya madini pekee, pamoja na kutilia mkazo kwenye vyanzo ambavyo vilionyesha kutokufikia lengo kwenye ukusanyaji wa mapato ili kuwe na tija kwenye zoezi hilo.
Naye Katibu Tawala wa Wilaya, Bi. Lucy Beda, aliagiza Idara za Biashara kutoka Halmashauri zote mbili, kuongeza usimamizi pamoja na ufuatiliaji wa leseni za biashara ili kudhibiti upotevu wa mapato, huku pia akisisistiza suala la uwajibikaji na ufanyaji wa kazi kwa kushirikiana miongoni mwa Idara na Vitengo huskia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Ndg. Karia Magaro, amewataka watumishi kufanya kazi kwa weledi na nidhamu ili lengo la ukusa yaji wa mapato liweze kufikiwa, pamoja na kuziagiza Idara na Vitengo vinayohusika na ukusanyaji wa mapato kuwasilisha taarifa sahihi ya hali ya ukusanyaj kwenye maeneo yao.
Awali wakati akisoma taarifa ya jumla ya Ukusanyaji wa Mapato ya Halmashauri ya Wilaya, Geita, Mwekahazina Bi. Eveline Ntahamba amesema kuwa, ili kufikia lengo la Bilioni 14 kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ambalo Halmashauri imejiwekea, Halmashauri imejipanga kuogeza timu ya wakusanya mapato pamoja na kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Kikosi Kazi cha Ukusanyaji wa Mapato.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa