Halmashauri ya Wilaya ya Geita imetoa kiasi cha shilingi milioni 177, kwa vikundi vya wanawake, vijana pamoja na watu wenye ulemavu, vyenye jumla ya wanachama 460, kwa kipindi cha robo ya tatu (Januari hadi machi, 2019).
Fedha hizo zimetolewa katika pesa iliyotengwa na Halmashauri shilingi milioni 330 kwa ajili ya kutoa mikopo kwa vikundi hivyo, katika mwaka 2018/2019 ikiwa ni kutokana na mapato ya ndani asilimia ya 10% ambapo wanawake watapata 4%, vijana 4% na watu wenye ulemavu 2%.
Akizungumza katika zoezi la muendelezo wa kusaini mkataba wa mkopo pamoja na kutoa hundi kwa vikundi hivyo kwa robo ya tatu, Kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Geita Donald Nssoko amesema mkopo huo ulianza kutolewa kwa vikundi toka Julai hadi Disemba 2018.
Aidha amesema Halmashauri imetoa muda wa nyongeza wa mwezi mmoja zaidi kwa vikundi kurejesha mikopo, hivyo baada ya kurejesha fedha hizo ndani ya kipindi cha miezi 3, watarejesha kwa miezi 4.
Mratibu Afisa Maendeleo ya Jamii Mathelina Mgina ameongeza kuwa Halmashauri ya Wilaya imeamua kuongeza muda wa kurejesha mkopo huo kwa vikundi,ikiwa ni kuunga mkono sera ya viwanda, kwa kuwa baadhi ya vikundi vinajishughulisha na viwanda vidogo vidogo hivyo Halmashauri imetoa muda wa ziada ili viweze kufanya maandalizi ya uzalishaji wa bidhaa zao.
Hata hivyo Mgina amesema pamoja na mafanikio ya watu hasa wenye ulemavu kuhamasika kujiunga kwenye vikundi kwa lengo la kujiongezea kipato, lakini bado kuna changamoto ya mwitikio mdogo wa kujiunga kwenye vikundi kwa baadhi ya vijana wa bodaboda,wavuvi pamoja na wachimbaji madini.
Akiongea kwa niaba ya vikundi mwenyekiti wa kikundi cha Nyarugusu Women Miners Donatha Yakubona, ameishukuru Halmashauri ya Wilaya pamoja na Serikali kwa ujumla kwa kutoa milioni 177 kwa ajili ya kuwawezesha na kuahidi kutumia fedha hizo za mkopo kwa malengo yaliyokusudiwa pia kuzirejesha ndani ya muda uliopangwa.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa