Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Rosemary Senyamule akiwa katika ziara ya kikazi Aprili 25, 2022 katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita amepokea mashuka 30, vitanda 10 na magodoro yake, viti 50, meza 50 pamoja na madawati 50 kutoka Benki ya NMB, vyenye thamani ya shilingi milioni 30 kwa ajili ya shule 5 na kituo cha Afya katoro.
Akipokea vifaa hivyo katika hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika katika kituo cha Afya Katoro Mhe. Senyamule ameishukuru Benki hiyo ya NMB kwa kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita katika kuboresha huduma za jamii huku akitoa wito kwa wanafunzi kutambua wajibu wao ni kusoma kwa bidii ili wafaulu vizuri na baadae kuja kulitumikia Taifa katika nafasi mbalimali.
Kwa upande wake Meneja wa Benki ya NMB kanda ya ziwa Bw. Baraka Ladislaus amesema kuwa Benki hiyo imekuwa na utaratibu wa kusaidia huduma za jamii hasa katika miradi ya Elimu na Afya huku akizungumzia ufadhili wa masomo ya kidato cha tano na sita na elimu ya juu kwa wanafunzi wanaofaulu vizuri na wanaotoka kwenye mazingira magumu unaotolewa na Benki hiyo.
Walimu wakuu wa shule zilizopokea misaada hiyo wameishukuru Benki ya NMB kwa kuwapatia samani hizo ambazo zitasaidia kupunguza msongamano katika shule hizo ambazo zimekuwa na wanafunzi wengi huku wakiomba wadau wengine pia kuendelea kujitolea vifaa hitajika katika miundombinu ya elimu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita John Wanga akijibu changamoto za miundo mbinu ya kituo cha Afya katoro zilizotolewa na Mganga Mfawidhi wa kituo hicho Dr. Rhoda Haule amesema kuwa kukamilika kwa Mradi wa Hospitali ya Wilaya katoro unaoendelea kwa sasa kutapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto zinazokikabili kituo hicho cha Afya na kuboresha huduma kwa wananchi wote wa Katoro na maeneo jirani.
Aidha Mkurugenzi Wanga ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa Bilioni 2.2 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali hiyo sambamba na kiasi cha shilingi milioni 600 zilizotolewa kwa ajili ya Mradi wa kupanga, kupima na kumilikisha Ardhi, fedha zilizotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Msaada huo uliotolewa na Benki ya NMB umezinufaisha Shule ya Sekondari Bahari na shule za Msingi Msufini, Mtakuja, Magenge, Mchongomani, pamoja na kituo cha Afya Katoro.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa