Na. Michael Kashinde
Wito umetolewa kwa wananchi na viongozi wa kata ya Lwamgasa kuhakikisha hakuna mtoto anayeshindwa kwenda shuleni kwa visingizio vyovyote ikiwemo michango mbalimbali, kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuboresha miundombinu ya Elimu na kutoa Elimu bila malipo ili kumsaidia kila mwanafunzi apate Elimu bora katika mazingira bora bila kuathiriwa na changamoto kama hizo.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela ametoa wito huo May 6, 2023 wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Lwamgasa katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la zahanati ya Lwamgasa ambapo amesema kuwa michango yoyote ile isizuie mtoto kwenda shule na kama kuna utaratibu wa kuchangia chochote lazima kwanza ashirikishwe Mhe. Mkuu wa Wilaya.
RC Shigela ameendelea kusema kuwa dhamira ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuona kila mtanzania anapata huduma bora za msingi ikiwemo Elimu na Afya na ndio maana kwa kuangalia hilo ametangaza ajira zaidi ya 12,000 katika Sekta hizo za Afya na Elimu ili kuongeza nguvu katika kuwahudumia watanzania, huku miundombinu ya umeme, maji na barabara ikiendelea kuboreshwa pia.
Amewasisitiza wananchi hao ambao wengi wao wanajihusisha na shughuli za uchimbaji mdogo wa madini ya dhahabu kuwapeleka watoto wao shule ili wasome na kupata ujuzi wa kitaalamu ili miaka ijayo waweze kuwa wataalamu katika sekta mbalimbali na hata wakiendelea kufanya shughuli za uchimbaji basi wawe wachimbaji na wawekezaji wakubwa kwa maendeleo ya Taifa lao.
Ametoa rai pia ya kuwalinda watoto wa kike ili wasome na kufikia malengo yao badala ya kuwalaghai kimapenzi na kuwaharibia maisha huku akiwasisitiza kuwa na maelewano ya kimkataba kati ya mwenye ardhi na mwekezaji katika eneo husika kwa njia ya fidia au makubaliano mengine yanayoeleweka ili kila mmoja anufaike kwa nafasi yake, huku akiahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuwarisishia njia mbalimbali za kufanya shughuli zao ikiwemo upatikanji wa leseni.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita ACP. Safia Jongo ametoa rai kwa wananchi hao kutojichukulia sheria mikononi katika kutatua masuala mbalimbali badala yake wavishirikishe vyombo vya dola vyenye jukumu la kusimamia masuala ya kiusalama huku akisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wale wote wanaojihusisha kwa uvunjifu wa amani kupitia ushirikiana wakiwemo baadhi ya waganga wa kienyeji.
Katika kukomesha matukio ya kutoa na kupokea rushwa ACP. Safia amezungumza na wananchi wa Kata ya Lwamgasa akiwaambia kuwa huduma ya dhamana katika vituo vya Polisi ni bure hivyo mwananchi yeyote akiombwa fedha ya dhamana katika kituo cha Polisi asikubali huku akitoa namba zake za simu kwa wananchi hao ikiwa ni njia rahisi ya kuwasaidia kwa haraka endapo kuna matukio yoyote ya uvunjifu wa amani.
Akiwa katika ziara yake ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita RC. Shigela alianzia katika kata ya Lwamgasa kwa kuzindua na kuweka jiwe la Msingi katika shule ya Sekondari Msisi zoezi lililoambatana upandaji miti katika viwanja vya shule hiyo, kabla ya kuelekea kuzindua kiwanda cha kuchakata Dhahabu cha Isra ziara iliyohitimishwa katika eneo la zahanati ya Lwamgasa kwa ukaguzi wa zahanati hiyo na mkutano wa hadhara sambamba na kujibu kero mbalimbali za wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Cornel Magembe akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kiwanda cha kuchakata Dhahabu cha Isra amesema kuwa Serikali inaendelea kuwasaidia wawekezaji kufanya kazi katika mazingira salama na wezeshi ili kulinda mitaji yao huku akiendelea kuhamasisha ushirikiano kati ya wananchi na wawekezaji ili kuendelea kutengeneza fursa za ajira kwa maendelea ya wananchi wa maeneo husika na taifa kwa ujumla.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa