Halmashauri ya Wilaya ya Geita imejiwekea mikakati mahususi ya kukabiliana na matumizi holela ya mifuko ya plastiki, ikianza na maeneo ya soko la CCM Katoro, ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Wiki ya Mazingira Duniani.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa wiki hiyo Mei 31, 2025, katika viwanja vya CCM Katoro, Mkuu wa Kitengo cha Maliasili na Hifadhi ya Mazingira katika halmashauri hiyo, Bw. David O. Mlahagwa, amesema kuwa hatua madhubuti zitachukuliwa kwa watakaobainika kutumia mifuko hiyo kinyume cha sheria.
“Mkakati wetu wa kwanza ni kufanya ukaguzi katika maduka yote. Tukikuta mtu anatumia mifuko ya plastiki, tutamchukulia hatua za kisheria. Pili, tutadhibiti aina ya mifuko inayotumika kama vifungashio ambayo huruhusiwa, lakini haitakiwi kurudi kwa wananchi baada ya matumizi,” amesema Mlahagwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Ndg. Karia Magaro, amewataka wafanyabiashara wa soko la Katoro kuendeleza jitihada za usafi katika maeneo yao.
“Niendelee kuwaomba tuhamasishane, na kila mmoja ahakikishe eneo lake linafanyiwa usafi,” amesisitiza Magaro.
Akihitimisha, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mhe. Hashim Komba, ametoa rai kwa wananchi kutokutupa ovyo bidhaa za plastiki na kuacha kabisa matumizi ya mifuko hiyo.
“Tusitupe chupa wala mifuko ya plastiki hovyo. Plastiki haitooza; itatuharibia mazingira yetu, na baadaye mazingira hayo yatatuathiri sisi wenyewe,” amesema Komba.
Uzinduzi huo ulitanguliwa na zoezi la usafi katika maeneo ya soko hilo, likishirikisha watumishi wa halmashauri, wafanyabiashara na wakazi wa eneo hilo.
Maadhimisho ya Wiki ya Mazingira Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 5 Juni, kufuatia uamuzi wa mwaka 1972 wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP), linalolenga kuhamasisha ulinzi wa mazingira duniani kote.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa