Na Michael Kashinde
Katika kumsaidia mkulima kufanya kilimo chenye tija, Halmashauri ya Wilaya ya Geita imeanzisha mkakati wa kila Kata kutilia mkazo zao moja ambalo wakulima wa Kata husika watalima kwa umahiri zao hilo ili liweze kuwapa tija.
Hayo yamebainishwa katika taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Adv. John Wanga, iliyowasilishwa na Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Katoro Damian Aloyce Septemba 8, 2022 katika mkutano wa baraza la madiwani kwa kipindi cha robo ya nne kati ya Aprili hadi Juni 2022.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa Timu ya Menejimenti na Serikali ya Wilaya ya Geita imeamua kuja na mkakati huo ikiamini kuwa mkakati huu ukisimamiwa na kuhimizwa vizuri na viongozi katika Kata zote, mazao ya Pamba, Mahindi, Alizeti, Nanasi, Mpunga, viazi vitamu, na muhogo yataweza kuinua hali ya uchumi wa wakulima kwa kuwapatia kipato.
Kupitia mkakati huu Halmashauri inakusudia kuanzisha masoko ya kuuzia mazao hayo, suala litakalosaidia kuwapunguzia wakulima usumbufu wa kuuzia mazao yao shambani au kando kando ya barabara mbalimbali.
Aidha mkakati huu wa Kata moja zao moja la kimkakati, utawawezesha wakulima kupata mikopo toka taasisi za kifedha, kwa sababu watatambulika kuwa ni wazalishaji wakubwa wa mazao hayo.
Mkakati huo pia utaisaidia Halmashauri kuwa na uwezo wa kukusanya kwa urahisi mapato yatokanayo na ushuru wa mazao, tofauti na ilivyo sasa hivi ambapo gharama kubwa inatumika katika kukusanya mapato hayo.
Baraza la madiwani katika siku yake ya pili baada ya kipindi cha maswali na majibu limepokea na kupitisha taarifa za shughuli zilizotekelezwa na idara mbalimbali kwa kipindi cha robo ya nne kwa mwaka 2022, huku baraza hilo likimchagua Mhe. Hadija Said kuendelea kuwa makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Geita sambamba na kuchagua viongozi wa kamati mbalimbali.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa