Na Michael Kashinde
Kamati ya uelimishaji, uhamasishaji na ushirikishwaji wa jamii kuhusu kujikinga na magojwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita katika kikao chake cha Aprili 14, 2023 imeazimia kulifanya suala la Elimu ya Afya kwa Umma, kuwa ajenda ya kudumu katika vikao vya maendeleo ya kata na vijiji ili kuwajengea wananchi uelewa wa namna ya kujikinga na magonjwa mbalimbali yakiwemo ya milipuko.
Kamati hiyo inayoundwa na jumla ya wajumbe 45 kwa ngazi ya Halmashauri ambao ni wataalamu na viongozi mbalimbali katika jamii inaamini kuwa kutekelezwa kwa azimio hilo kikamilifu kutaisaidia jamii kupata Elimu ya kujikinga na magonjwa mbalimbali yakiwemo ya milipuko ambayo wakati mwingine yanaweza kusababishwa na uzembe au uelewa mdogo wa baadhi ya watu katika Jamii.
Bw. Ezrael Tarimo Afisa mifugo Halmashauri ya Wilaya ya Geita akitoa ufafanuzi wa namna idara ya Kilimo pamoja na mifugo zinavyoshiriki katika kuikinga jamii na magonjwa ambayo wakati mwingine husababishwa na hali za afya za wanyama hao au matumizi ya dawa muda mfupi kabla ya kuchinjwa, amefafanua kuwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita kuna utaratibu mzuri wa kukagua wanyama na kujiridhisha kabla ya kutoa vibali vya kuwachinja unaosimamiwa na wataalamu wa mifugo kwa lengo la kudhibiti hali hizo.
Bw. Tarimo ameendelea kusema kuwa utaratibu huo hautofautiani na unaotumika katika idara ya kilimo huku akitoa rai kwa jamii kutoa ushirikiano kwa wataalamu wa idara hizo katika jamii zao pale wanapoona baadhi ya wakulima au wafugaji wanakiuka taratibu hizo ikiwemo kupulizia dawa muda mfupi na kupeleka mazao sokoni ili kuikinga jamii kuathirika na madhara kama hayo.
kwa upande wake Afisa uelimishaji, uhamasishaji na ushirikishwaji jamii kutoka Wizara ya Afya sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma Bi. Magdalena Dinawi, akieleza majukumu ya kila mjumbe katika kamati hiyo katika ukumbi wa Hospitali ya Wilaya Nzera, amemtaka kila mjumbe kwa nafasi yake kuwajibika kikamilifu kwa kufikisha Elimu sahihi kwa jamii ili kuongeza uelewa zaidi kuhusu kujikinga na magonjwa.
Aidha Bi. Dinawi amewataka wajumbe wa kamati hiyo kuanza kutekeleza majukumu yao kuanzia sasa kwa kuandaa mipango kazi, kutoa misaada ya kitaalamu kwa wajumbe na jamii kwa ujumla ili kujenga uwezo wa kufanya usimamizi wa kazi zote za Kamati hiyo sambamba na kuisaidia jamii na kuiwezesha kushiriki shughuli mbalimbali yakiwemo majanga na dharura.
Naye mratibu wa kamati hiyo Halmashauri ya Wilaya ya Geita Bi. Frida Mkwama akizungumza wakati wa kikao hicho amesisitiza kuwa Elimu ya Afya ni tiba nzuri, huku akitoa wito kwa wajumbe hao wakiwemo viongozi wa dini ambao jamii inawaamini kwa kiasi kikubwa, kutumia majukwaa yao na nyumba za ibada kutoa Elimu hiyo ya Afya kwa jamii ili Elimu hiyo iwafikie wananchi wote na kwa njia rahisi.
Kamati hii ina jukumu kubwa la kuielimisha jamii, kuihamasisha na kuishirikisha kuhusu kujikinga na magonjwa mbalimbali hasa katika nyakati hizi ambazo karibia kila kukicha hapa duniani yanaibuka magonjwa ya milipuko, hivyo basi jukumu hili halibaki tu kwa kamati bali kila mmoja kwa nafasi yake anawajibika kujikinga na kuwakinga wengine pia kwa kufuata taratibu mbalimbali zinazoshauriwa na wataalamu ili kujiweka katika mazingira salama kwa kuwa hata mimi binafsi naamini kuwa Afya bora ni Msingi wa maendeleo ya mtu binafsi na taifa kwa ujumla hivyo tunawajibika kulinda Afya zetu..
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa