Na. Michael Kashinde
Wakati ambapo Mkoa wa Geita unatarajia kuadhimisha Siku 16 za kupinga ukatili, kwa kuongozwa na kaulimbiu isemayo ‘’Kila Uhai una thamani, Tokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto’’ Halmashauri ya Wilaya ya Geita imepanga kufanya uzinduzi wa maadhimisho hayo Novemba 29, katika Kata ya Katoro, ambapo mgeni rasmi atakuwa Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Wilson Samwel Shimo.
Siku 16 za maadhimisho hayo zinaanza Novemba 25, hadi Disemba 10, 2022 ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa kupinga ukatili wanatarijia kutumia siku hizo kutekeleza shughuli mbalimbali kama vile kuandaa mijadala na wanafunzi mashuleni, kuelimisha jamii kupitia vipindi vya radio na kutoa Elimu ya Saikolojia kwa wahanga wa masuala ya akili katika maeneo mbalimbali.
Shughuli nyingine zitakazotekelezwa katika maadhimisho hayo ni pamoja na huduma za kisheria zitakazofanyika katika wiki ya Msaada wa kisheria, huku Shirika la Voluntary Service Overseas (V.S.O) likipanga kufanya mdahalo na wanaume tu (Men’s Talk) Novemba 25 katika Kata ya Nyarugusu, ambapo wanaume wamelengwa katika mdahalo huo kwa kuwa wanaume wanaonekana kuwa wahusika wa ukatili katika jamii.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya jamii Halmashauri ya Wilaya ya Geita Bw. Alex Herman Novemba 24, 2022 akiwa na wadau hao wa kupinga ukatili katika kikao cha kujadili utekelezaji wa shughuli mbalimbali zitakazofanyika katika siku hizo za maadhimisho hayo ametoa wito kwa wadau hao kusaidia pia ukatili dhidi ya watoto wa kiume.
Bw. Alex amesema kuwa ni vyema jamii ikawa karibu na kufuatilia nyendo za watoto wa kiume pia kuanzia mashuleni kwa kuhamasisha uangalizi wa karibu ili kuwaepusha watoto hao kufanyiwa ukatili ambao unachangiwa na mmomonyoko wa maadili, hali inayopelekea pia kuongezeka kwa matendo vya mapenzi ya jinsia moja suala ambalo ni mmomonyoko mkubwa wa maadili.
Maadhimisho hayo ya kupinga ukatili kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita yanatarajia kuwashirikisha wadau na mashirika mbalimbali wakiwemo Plan International, Nelico, Kivulini, V.S.O, Sedit, Patwao, Rafiki SDO, Gelac na Bright Light.
Aidha wadau na mashirika mengine ni pamoja na Gelao, Marafiki wa Elimu, Mwanasheria Geita DC, .Polisi dawati la Jinsia, TWCC Jinsia na The Golden Line (Walter).
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa