Serikali kupitia Mpango wake wa kunusuru kaya masikini wa TASAF imekuwa ikitoa kiasi cha Shilingi 11,036,000 kila awamu kwa ajili ya kusaidia jumla ya kaya 267 za vijiji vya Ntinachi na Nyawilimilwa ambapo fedha hizo zimewasaidia wanufaika hao kujikimu katika mambo mbalimbali ya maendeleo.
Bi. Anicia Mwanzalima Nyanda akiwasilisha taarifa ya walengwa hao wa TASAF kwa Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Wilson Shimo Juni 11, 2022 amesema kuwa kupitia fedha hizo kaya 6 zimefanikiwa kunua mabati ya kuezekea nyumba zao, kaya 10 zimenunua mbuzi, huku kaya 2 zikifanikiwa kuchimba visima vya maji.
Bi. Anicia ametaja mafanikio mengine ni pamoja na kaya 17 kuazisha miradi ya ufugaji wa kuku wa kienyeji, huku kaya nyingine zikianzisha ujenzi wa nyumba na vyoo, ambapo pia wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwakumbuka na kuwapatia pesa ili kuondoa umasikini.
Akizungumza na wanufaika hao Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Wilson Shimo amewapongeza wanaotumia fedha hizo kufanyia shughuli za maendeleo katika familia zao huku akitoa rai ya kuwa na matumizi mazuri ya fedha hizo badala ya kutumia kwa ulevi sanjari na kuwakumbusha wanufaika hao kujifunza kusoma, kuhesabu, na kuandika ili kujua kiasi cha fedha kila mmoja anachotakiwa kupokea ambapo amewachangia fedha kwa ajili ya kununua madaftari ya kujifunzia.
Katika kila awamu ya malipo ya TASAF kiasi cha shilingi 3,818,000 kimekuwa kikitolewa na Serikali kwa ajili ya kusaidia kaya 100 katika kijiji cha Ntinachi, huku jumla ya Shilingi 7,218,000 zimekuwa zikitolewa kusaidia kaya 167 zilizopo katika kijiji cha Nyawilimilwa.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa