Na Michael Kashinde
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Wilson Shimo amewataka viongozi na watumishi mbalimbali wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita kuwahamasisha wananchi kufanya kilimo cha kisasa ili kuongeza uzalishaji huku akisisitiza kuwa na tahadhari katika kuuza mazao hayo ya chakula ili kubaki na ziada ya kutosha katika matumizi ya chakula katika ngazi za familia.
Mhe. Shimo ameyasema hayo Septemba 6, 2022 akiwa katika siku ya kwanza ya mkutano wa nne wa kawaida wa baraza la Madiwani kwa mwaka wa fedha 2021/2022 uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Nzera ambapo mkutano huo umepokea na kupitisha taarifa za utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa kipindi cha Mwezi Aprili hadi Juni 2022.
Mhe. Shimo amesema kuwa ni vyema wananchi wakahamasishwa kufanya kilimo cha biashara huku akieleza kuwa kuna mchakato maalumu wa kilimo unaoandaliwa ambapo kila Kata itahamasishwa na kuwa na zao lake kuu litakalolimwa katika eneo husika suala litakalosaidia katika kuongeza ubora, uzalishaji, kuitangaza kata husika pamoja na kurahisisha masoko ya mazao hayo.
Aidha DC Shimo ametumia nafasi hiyo kutoa rai kwa viongozi na watumishi mbalimbali kuwakumbusha wananchi kuuza vyakula kwa kiasi ili wabaki na ziada ya chakula katika familia zao, kwa kuwa mamlaka za hali ya hewa zimetoa taarifa ya uhaba wa mvua kwa mwaka huu hali inayoleta hofu ya njaa ingawa mpaka sasa bado Wilaya ya Geita ina chakula cha kutosha.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mhe. Charles Kazungu ameshukuru kwa kusema kuwa baraza lake limepokea ushauri uliotolewa na viongozi mbalimbali wa Wilaya na kusisitiza kuwa ni jukumu la madiwani kuwahamasisha wananchi kufuata maelekezo ya viongozi mbalimbali Serikali kwa kutumia vikao vyao vya maendeleo ya Kata.
Mhe. Kazungu ameendelea kwa kusema kuwa suala la kilimo cha aina moja katika kila Kata ni suala jema ambalo litasaidia Kata hizo kutambulika kwa uzalishaji wa mazao husika yatakayokuwa yakilimwa katika maeneo hayo.
Wakati huo huo Madiwani mbalimbali wakiwasilisha taarifa za utekelezaji wa maendeleo katika Kata zao kuhusu Sekta ya kilimo wamesema kuwa wananchi wamehamasika kulima mazao mbalimbali ya chakula na biashara kama vile Mahindi, Maharage, Pamba, viazi vitamu, mihogo, ndizi, na mengine mengi.
Kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa maendeleo katika Kata ya Isulwabutundwe iliyowasilishwa na diwani wa Kata hiyo Mhe. Maweda Gwesandili amesema kuwa wakulima waliolima mazao ya biashara na chakula tayari wameanza kuvuna ambapo kwa sasa bei ya mahindi ni Tshs. 68,000/= huku mpunga ukiwa ni Tshs. 90,000/= kwa gunia.
Kwa upande wa mazao ya biashara taarifaya Kata hiyo imeeleza kuwa wananchi wengi walihamasika kulima zao la pamba ambapo mpaka sasa wamefanikiwa kuvuna pamba hiyo kiasi cha Kg 29,819 na kuipeleka katika maghala ambapo wamekuwa wakiuza kwa bei ya kati ya Tshs. 1800 na Tshs. 1900 kwa kilo.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa