Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe.Wilson Shimo Aprili 5, 2022 amejitolea pesa kwa ajili ya kununua kalamu na madaftari kwa wanufaika wa TASAF katika kijiji cha Chigunga ili wahamasike kujifunza kusoma na kuandika.
Mhe.Shimo alifanya ziara katika vijiji vya Isima na Chigunga vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita ili kukagua utekelezaji wa mpango wa kunusuru kaya masikini TASAF na kuzungumza na wanufaika wa mpango huo.
Baada ya kuzungumza na wanufaika hao alibaini kuwa wengi wao hasa wazee hawajui kusoma na kuandika hivyo kuwahamasisha kujifunza stadi hizo ili wafahamu taarifa muhimu zinazowahusu wao wenyewe ikwemo kiasi cha fedha wanachotakiwa kukipata.
Mhe.Shimo amesisitiza kuwa elimu hiyo itawasaidia pia kuepuka mapunjo yoyote wanayoweza kuyapata kwa sasa bila ya wao kujua, kutoka kwa mawakala wa malipo au hata ndugu wanaowatuma kuwapokelea fedha hizo huku akiwataka kutoa taarifa pale wanapohisi kudhulumiwa.
Akiwa katika kijiji cha Chigunga ameshauri kutafuta mwalimu Mstaafu ambaye anaweza kutumia muda mfupi tu kwa kila siku kuwafundisha wanufaika wasiojua kusoma na kuandika huku akitoa fedha taslimu kwa ajili ya kununua kalamu na madaftari, sambamba na kumteua kiranja mkuu, kazi ikibaki kwao ya kutafuta mwalimu wa kuwafundisha.
kwa upande wake mratibu wa Mpango huo wa kunusuru kaya masikini TASAF katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita Gabriel Evarist, amesema kuwa katika ziara hiyo ya Mkuu wa Wilaya wamebaini baadhi ya changamoto katika taratibu za malipo ya mwezi wa kwanza na wa pili huku akiahidi kuzishughulikia haraka iwezekanavyo.
Katika taarifa zao kwa Mkuu wa Wilaya zilizowasilishwa na Victoria Malima Nyakina na Benziless Mayengo Wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha hizo ambazo zimewasaidia katika shuguli za kilimo na ufugaji, biashara ndogo ndogo, kuboresha makazi na kuwasomesha watoto.
Kijiji cha Isima chenye vitongoji vinne kina walengwa 146 ambapo kwa kipindi cha Julai 2015 hadi Machi 2022 kimepokea jumla ya Tshs.180,436,480/= ambazo zimelipwa kwa walengwa, huku kijiji cha Chigunga chenye walengwa 122 ambacho kimeingia kwenye mpango Januari 2022, kimepokea jumla ya Tshs.15,970,000/= malipo ya awamu mbili.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa