Na Michael Kashinde
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe.Wilson Shimo akiwa na kamati ya ulinzi na usalama Wilaya, katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita Agosti 3, 2022 amewaweka ndani Mafundi na wasimamizi wa miradi ya TASAF baada ya kuonekana dosari zilizosababishwa na uzembe wao katika Miradi wanayoisimamia huku akiwataka wahusika hao kurekebisha haraka dosari hizo mara tu atakapowatoa.Waliokutana na adhabu hiyo ya Mhe. Shimo ni Bw.Stephen Kayogo ambaye ni fundi Mkuu Shule ya Msingi Makatani katika kijiji cha Ihumilo, Bw. Mathayo Mgongo ambaye pia ni fundi Mkuu katika Mradi wa Nyumba ya Mtumishi katika shule ya Msingi Nyamikoma kijiji cha Lwenge, Bw.Emmanuel Masondole ambaye ni Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Lwenge na Bw. Juma Richard ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya ujenzi katika mradi huo.
Mhe. Shimo akiwa na Kamati ya ulinzi na usalama Wilaya, ameanza ziara yake kwa kutembelea mradi wa ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa ofisi moja ya Mwalimu pamoja na matundu sita ya vyoo, uliotengewa kiasi cha Tshs.66,845,000/= ambapo nguvu za wananchi katika mradi huo ni Tshs.7,899,000/= ambapo kwa sasa mradi uko katika hatua ya kupauliwa kwa upande wa vyumba vya madarasa na ofisi ya Mwalimu.Baada ya kupokea taarifa na kukagua mradi huo Mhe. Shimo ametoa wiki mbili kwa wasimamizi wa mradi huo kuhakikisha wanawasiliana na Mzabuni wa vifaa ili avilete haraka na kazi iendelee huku akiitaka kamati ya ujenzi wa mradi huo kufuatilia kila hatua ya mradi na kurekebisha haraka dosari zilizojitokeza sambamba na kuwahamasisha wananchi kuchangia nguvu zao katika mradi huo ili shule zitakapofunguliwa uwe tayari kutumika.
DC Shimo ametembelea mradi wa ujenzi wa nyumba ya watumishi ya Two in One katika Zahanati ya Shilamena mradi uliofikia katika hatua ya kuelekea kupaua ambapo amewapongeza wasimamizi wa mradi huo kwa umakini na ubora unaoonekana katika mradi huo huku akitoa ushauri wa kuvuta umeme katika zahanati hiyo ambayo hivi karibuni itaanza kutoa huduma ili kuboresha na kurahisisha huduma mbalimbali hasa za uzazi.
Katika kijiji cha Lwenge kuna mradi wa mpango wa TASAF ambao ni ujenzi wa nyumba ya Mwalimu Two in One katika shule ya Msingi Nyamikoma ambao TASAF makao makuu wametoa kiasi cha 100,045,892 ikiwa ni 90% ya mradi husika huku nguvu za wananchi zikiwa ni 10% ili kuukamilisha.
Viongozi wa Mradi huo akiwemo fundi mkuu wametakiwa kurekebisha haraka dosari zilizobainishwa na Kamati hiyo ya ulinzi na usalama Wilaya sambamba na kuendelea kuhamasisha wananchi kutumia nguvu zao ili kuongeza kasi ya mradi huo.
Mathayo Kuzenza na Daniel Selemani wameishukuru Serikali chini ya Rais Samia kwa kuwaletea miradi hiyo ambayo imekuwa na tija kwa wananchi hao akitolea mfano wa kipindi cha nyuma wao walikwenda umbali mrefu kwa ajili ya kupata Elimu ingawa kipindi cha masika walishindwa kwenda kwa kuwa kulikuwa na mto uliokuwa unajaa na kuziba njia ambapo kwa sasa kwenye eneo lile la mto pamejengwa daraja na Shule imesogezwa katika kijiji chao.Akifunga siku ya kwanza ya ziara yake katika miradi ya TASAF katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mhe. Shimo amewataka wale wote waliopewa nafasi ya kusimamia na kujenga miradi hiyo kushiriki kikamilifu katika kutimiza wajibu huo ili miradi hiyo iwe na ubora unaotakiwa huku akisisitiza kuwa hatua anazozichukua dhidi ya wanaozembea ni katika kuwakumbusha kutekeleza wajibu wao kwa maslahi ya Taifa huku akimshukuru Rais Samia kwa kuipatia Wilaya ya Geita miradi mingi na yenye tija kwa wananchi.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa