Na. Michael Kashinde
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Wilson Shimo ametoa rai kwa wanawake na watoto katika jamii kuepuka migogoro katika familia ambayo inaweza kuchangia kufanyika kwa vitendo vya ukatili.
Amezungumza hayo Novemba 29, 2022 katika ukumbi wa JJ Katoro wakati akifungua maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita maadhimisho yaliyoanza Novemba 25 na kutarajiwa kuhitimishwa Disemba 10, 2022.
DC Shimo amesema kuwa hata wanawake wanapaswa kuacha ukatili kwa wanaume huku akitolea mfano baadhi ya lugha kali zinazotumiwa na wanawake dhidi ya waume zao ambazo wakati mwingine zinakuwa chanzo cha migogoro inayopelekea vitendo vya ukatili.
Wakati huo huo amewataka watoto pia katika familia kuacha chokochoko ambazo zinaweza kuwapunguzia uwajibikaji wakakosa heshima na adabu suala linaloweza kuchangia wazazi au walezi kutoa adhabu au vipigo vinavyotokana na hasira suala ambalo ni ukatili pia.
Aidha DC Shimo ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa kushirikiana na wadau wa kupinga ukatili kwa kuendeleza juhudi za kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kamati za kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika kata zote 37 za Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
Akitoa neno la shukrani kwa Mgeni rasmi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Adv. John Wanga amesema Halmashauri ya Wilaya ya Geita imepokea maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na mgeni rasmi huku akiahidi kushirikiana na wadau mbalimbali kuyasimamia mabaraza ya watoto ya kupinga ukatili ili yawe chachu ya kupeleka taarifa hizo katika jamii zetu.
Adv. Wanga ameendelea kwa kusema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Geita inaendelea kutoa mikopo ya asilimia 10 kwa makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ikiwa ni fursa ya kuwajengea uwezo wa kujitegemea ili wasiwe dhaifu kiuchumi.
Awali akitoa taarifa kwa mgeni rasmi Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita Bi. Enedy Mwanakatwe amesema kuwa kesi za ukatili ambazo zimekuwa zikipokelewa kutoka katika makundi mbalimbali ya kinamama na watoto ni pamoja na ukatili wa kisaikolojia, kimwili, kingono na kiuchumi ambapo kwa kipindi cha Mwezi Januari hadi Oktoba 2022 matukio yaliyotolewa taarifa ni 26 ambapo ubakaji ni matukio 7, ulawiti ni 2 na vipigo ni 17.
Bi. Mwanakatwe ameendelea kusema kuwa pamoja na matukio hayo kutolewa taarifa na wanawake na watoto lakini pia baadhi ya wanaume wamekuwa wahanga wa ukatili japokuwa hawatoi taarifa katika Ofisi hizo za maendeleo ya jamii suala ambalo linatia ugumu kupata taarifa zao sahihi.
Aidha Bi. Mwanakatwe amesema kuwa katika kutekeleza mpango kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto Halmashauri imefanikiwa kuunda mabaraza ya watoto na kamati za MTAKUWA ili kupambana na ukatili dhidi ya wanawake na watoto huku akiwashukuru wadau wanaoshirikiana na halmashauri kufanikisha juhudi hizo.
Maadhimisho hayo yameanza na maandamano ya hiyari katika Kata ya Katoro yakiwashirikisha wananchi na wadau mbalimbali waliokuwa na mabango ya jumbe za kupinga ukatili ambapo pia elimu ya Kupinga ukatili imetolewa kwa wananchi waliojitokeza.
Miongoni mwa mashirika ambayo ni wadau wakubwa wa kupinga ukatili wanaofanya kazi na Halmashauri ya Wilaya ya Geita ni pamoja na PLAN International, VSO, PATWAO, Dawati la jinsia kutoka jeshi la Polisi, SEDIT, Marafiki wa elimu,Bright Light, Gelao na SMAUJATA.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa