Na. Michael Kashinde
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Wilson Samwel Shimo ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa mpango wake wa kuanzisha shule mpya za sekondari badala ya kuongeza majengo ya vyumba vya madarasa katika shule zilizopo hali inayofanya kuwa na majengo mengi katika shule moja.
DC Shimo ametoa pongezi hizo Oktoba 28, 2022 akiwa katika mkutano wa kawaida wa baraza la madiwani kwa robo ya kwanza kwa mwaka wa fedha 2022/2023 uliofanyika Oktoba 27 na 28 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Nzera.
Ameendelea kusema kuwa kuanzishwa kwa shule mpya hizo kunapunguza changamoto ya shule moja kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi kuliko kawaida lakini pia ni msaada mkubwa kwa wanafunzi kwa kuwa hawataathirika na umbali kutoka nyumbani kwenda shuleni kila siku.
Wakati huo huo Mhe. Shimo ametoa rai kwa Halmashauri na madiwani kuhakikisha wanafuatilia kwa karibu mabaraza ya kazi, utendaji wa viongozi wake na namna yanavyofanya kazi kwa ujumla sambamba na kuyasaidia pale yanapohitaji msaada zaidi, huku akiwakumbusha pia kutoa taarifa katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya pale wasikiapo malalamiko ya rushwa kutoka kwa wananchi katika shughuli za utendaji wa Mahakama za mwanzo.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Geita Barnabas Mapande baada ya kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa fedha za ujenzi wa madarasa ya shule za sekondari, ametoa wito wa kusimamia vizuri ujenzi wa vyumba hivyo 267 vinavyojengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita na kuvikamilisha kwa wakati huku akisisitiza kuwa, kwa kufanya hivyo ni kumuunga mkono Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan aliyeguswa kuwasaidia watoto wengi wa hali ya chini kwa kuwajengea miundombinu bora na ya kisasa.
Aidha ametumia nafasi hiyo kuwaomba viongozi mbalimbai watakaotakiwa kutoa ushirikiano katika kufuatilia malipo ya watumishi waliotolewa kazini kwa mchakato wa vyeti feki kufanya hivyo, ili kuwasaidia watumishi hao kupata haki yao, huku akiendelea kuzitaka mamlaka husika kuzuia wananchi mapema wanapotaka kuanza kulima katika maeneo yaliyozuiwa na Serikali badala ya kuchelewa na kuja kufyeka tayari yakiwa chakula.
Naye mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mhe. Charles Kazungu ametoa wito kwa madiwani kushirikiana na watendaji wa maeneo yao katika kusimamia vizuri miradi ya mendeleo ambayo inaendelea kujengwa katika kata zao kwa kuzingatia ubora unaotakiwa kuanzia kwenye ununuzi wa matofali na vifaa vingine vinavyotumika katika ujenzi.
Aidha amesisitiza kuwa Halmashauri imepokea ushauri uliotolewa na wajumbe na viongozi mbalimbali kuhusu mambo yote yaliyojadiliwa kwa siku mbili za mkutano huo, huku akiwataka madiwani kuona umuhimu wa kupata gari la zimamoto kwa ajili ya kudhibiti ajali za moto hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali inajenga miradi mikubwa na yenye kutumia fedha nyingi kwa kuwa mpaka sasa Halmashauri haina gari la zimamoto.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Adv. John Wanga akijibu hoja mbalimbali zilizojadiliwa katika mkutano huo amesema kuwa katika kudhibiti suala la ujenzi holela Timu ya Menejimenti inaandaa andiko kwa ajili ya kuweka utaratibu wa matumizi bora ya ardhi ili kudhibiti ujenzi holela katika maeneo yanayokua kwa kasi.
Aidha Adv. Wanga amefafanua kuwa Timu ya Menejimenti imebaini kuwa ujenzi huu holela unasababishwa na uuzwaji wa ardhi kiholela katika maeneo yanayokua kwa kasi kutokana na uwepo wa huduma ya umeme wa REA ambapo Halmashauri imeamua kuja na mkakati wa kuunda kamati ndogondogo za usimamizi wa ardhi ambazo zitahakikisha mwananchi anayepata eneo kwa sasa anajenga bila kukosea.
Uwepo wa nishati ya umeme kwenye maeneo ya vijijini kupitia mpango wa REA umeleta mabadiliko makubwa katika maeneo hayo kwa kuwa yamekuwa yakikua kwa kasi na kukua kwa huduma mbalimbali za kijamii suala ambalo linawavutia pia watu wengi kuwekeza katika maeneo hayo ambapo kwa kuliona hilo Halmashauri ya Wilaya ya Geita imeona kuna haja ya kuchukua hatua mapema.
Katika mkutano wa siku mbili wa robo ya kwanza kwa mwaka wa fedha 2022/2023 baraza la madiwani limekamilisha shughuli mbalimbali ikiwemo kupokea na kupitisha taarifa za utekelezaji wa shughuli za maendeleo kuanzia ngazi za kata, taasisi na Idara mbalimbali, sambamba na taarifa za kamati mbalimbali za kudumu, huku pia maswali mbalimbali ya waheshimiwa madiwani yakitolewa majibu.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa