Baraza la madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya geita limeshauriwa kuwa na umoja na ushirikiano katika kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo, na kukosoana kwa kusaidiana katika vikao na mabaraza halali pale panapotokea tofauti za kiutendaji.
Wito huo umetolewa Februari 3, 2022 na mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe.Wilson Shimo wakati akizungumza na wajumbe wa mkutano wa kawaida wa baraza la madiwani wa robo ya pili kwa mwaka wa fedha 2021/2022 katika siku ya pili ya kikao katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Nzera.
Mhe. Shimo amesema kuwa siri ya mafanikio katika utendaji ni umoja na ushirikiano huku akiwataka wajumbe wa mkutano huo kushauriana na kusaidiana panapotokea tofauti mbalimbali kwa kuwa wote kwa pamoja wanaijenga Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa kuwatumikia wananchi.
Aidha amewashauri wajumbe hao wanapoona tofauti zozote ni bora kuitana katika vikao na kujadiliana ili kufikia maakubaliano yenye tija suala linaloweza kusaidia kupata maendeleo huku akiwataka kuwa na maamuzi ya pamoja katika maswala ya kimaendeleo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Geita Barnabas Mapande amezitaka Taasisi mbalimbali za kiserikali zinazohusika katika maendeleo kushiriki kikamilifu katika vikao vya kamati za kudumu ili kuongeza uelewa na kutoa nafasi ya kujadiliwa kwa taarifa za kamati hizo kwa upana.
Aidha ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia kwa namna alivyoiwezesha Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa fedha za miradi mbalimbali iliyo nje ya bajeti huku akiipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa namna ilivyofanikiwa kusimamia ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Naye mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mhe.Charles Kazungu amepongeza hatua ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Geita kuzitaka Taasisi mbalimbali kushiriki vikao vya kamati za kudumu za Halmashauri akiamini njia hiyo itasaidia kuongeza uelewa kwa pande zote sambamba na kupunguza muda wa majadiliano katika vikao vya mabaraza.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa