Na Michael Kashinde
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe.Wilson Shimo Agosti 4, 2022 amekabidhi pikipiki tano (5) kwa kikundi cha Mawemeru bodaboda group kilichopo katika kata ya Nyarugusu ukiwa ni mkopo uliotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Geita kuwasaidia vijana kujikomboa kiuchumi.
Mkopo huo una thamani ya shilingi 15,000,000/= ambapo umehusisha ununuzi wa pikipiki 5 kwa thamani ya shilingi 12,500,000/= huku kiasi cha shilingi 2,500,000/= kikitumika kwa ajili ya kununua vifaa vya kujikinga baridi na kingine kilichobaki kikitumika kama mtaji wa kuanzia.Mhe.Shimo akiwa ameambatana na kamati ya ulinzi na usalama Wilaya sambamba na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita amewapongeza vijana hao kwa ujasiri wa kufuata taratibu zote za kupata mkopo huo huku akitoa wito kwa waendesha bodaboda wote kufuata taratibu zote za usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanakuwa na Leseni na bima huku akiwakumbusha kutopuuzia kufunga vifaa ya kuzimia moto katika vyombo yao kama alivyoeleza awali Insp. Edward Lukuba Afisa Zimamoto Wilaya ya Geita akizungumza na madereva hao.Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Adv. John Wanga amesema kuwa kikundi hicho kilipitiwa na Mwenge wa Uhuru Julai 21 mwaka huu ambapo kiongozi wa mbio za Mwenge aliagiza kukata bima kubwa na leseni kwa kila dereva suala ambalo tayari limekamilishwa 100%.
Aidha Adv.Wanga ametumia pia nafasi hiyo kualika makundi mbalimbali wakiwemo vijana, wanawake na makundi maalumu kufuatilia utaratibu wa kupata mikopo isiyo na riba katika Halmashauri huku akisisitiza fedha hizo zipo kwa ajili yao ili kujikwamua kiuchumi.
Kwa upande wake Afisa vijana Halmashauri ya Wilaya ya Geita Bw. Alex Herman akizungumzia mkopo huo amesema kuwa ana matumaini ya kuona mafanikio kwa kikundi hicho kwa kuwa takwimu zinaonesha 90% ya vikundi vinayochukua mikopo ya bodaboda vimekuwa vikifanikiwa vizuri kwa kuwa vijana wa bodaboda hawana usumbufu katika marejesho.
Akizungumzia mkopo huo Bw.Leonard Nkalango ambaye ni mwanachama kikundi wa Mawemeru Group ameishukuru Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa kuwapatia mkopo huo bila riba pamoja na ushauri wa kitaalamu kuhusu upanuzi na usimamizi wa miradi ambapo pia ameeleza kuwa wamejipangia utaratibu kwa kukusanya kiasi cha shilingi 10,000/= kila siku kwa kila mmoja na kuweka kwenye Akaunti yao kwa ajili ya marejesho.Mawemeru bodaboda group ni kikundi kilichoanza rasmi mnamo mwaka 2021 kikiwa na mtaji wa shilingi 200,000/= tu ambazo walizitumia kukopeshana ili kujikwamua kiuchumi kabla ya kupatiwa mkopo wa shilingi 15,000,000/= ambapo rejesho lao la kwanza linatarajiwa kuwa Septemba 29 mwaka huu.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa