Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Wilson Shimo akiwa katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika ki Wilaya katika shule ya sekondari Lwezera Halmashauri ya Wilaya ya Geita Juni 16, 2022 amekemea ukatili mbalimbali unaofanywa na jamii kwa kujua ama kutokujua.
Mhe. Shimo ametumia maadhimisho hayo kuainisha vitendo mbalimbali vya kikatili wanavyofanyiwa watoto kwenye jamii zetu, huku akikemea vitendo hivyo na kuitaka jamii kushiriki kikamilifu katika malezi ya watoto ndani ya familia ili kuwalinda na mazingira mbalimbali hatarishi.
Miongoni mwa vitendo vya ukatili kwa Watoto alivyovikemea Mhe. Shimo ni pamoja na kutowapeleka shule na kufuatilia maendeleo yao, kuwapiga na kutoa adhabu kali, huku akisisitiza suala la kukaa shuleni muda mrefu bila kula ni ukatili pia na kuitaka jamii kuchukua hatua.
Aidha amemtaka kila mtu katika jamii kuhakikisha anatimiza wajibu wake kwa kuhusika kuwalea kimaadili watoto katika familia zao kuliko kuwaacha wakachangamana na watu wengine ambao wanaweza kuwa sio wema na kuwafunza mambo yasiyofaa katika jamii.
Mhe. Shimo ametumia nafasi hiyo Kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuonyesha kuwajali watoto na kuondoa ada kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita huku, huku akiendelea kuwahamasisha wananchi kushiriki katika zoezi la Sensa ya watu na makazi Agosti 23 na kutoficha taarifa zozote watakazoulizwa na makarani wa Sensa.
Naye Makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita na Diwani wa kata ya Nyamigota Bi.Khadija Said Joseph akizungumza katika maadhimisho hayo amewataka wananchi waliojitokeza hapo kuwa mabalozi wazuri kwa wenzao kwa kuwafikishia ujumbe wa siku ya Mtoto wa Afrika unaolenga kupinga ukatili na kuhamasika kushiriki katika zoezi la Sensa.
Awali Akisoma risala kwa Mgeni rasmi Anjelina Phinias Mwanafunzi wa Darasa la Sita katika Shule ya Msingi Lwezera ametaja changamoto mbalimbali wanazokutana nazo watoto ikiwemo ukatili wa aina mbalimbali ambao mara nyingine huanzia ngazi za familia kwa kukosa pia usimamizi mzuri wa wazazi.
Kwa upande wake Afisa Lishe Halmashauri ya Wilaya ya Geita Bi. Tibezuka Mapesa ametumia nafasi hiyo kuwahamasisha wananchi kuzingatia lishe bora hasa kuanzia ngazi za familia ili kuwasaidia watoto kukua vizuri kimwili na kiakili hali itakayosaidia kuepuka utapiamlo.
Maadhimisho hayo yameenda sambamba na burudani zenye jumbe mbalimbali kutoka katika vikundi mbalimbali ya watoto ambapo pia kulikuwa na zawadi kwa vikundi hivyo sanjari na kutoa misaada kwa watoto wenye uhitaji maalumu.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa