Na. Michael Kashinde
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Wilson Shimo akizungumza na wajumbe wa baraza la madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Geita Oktoba 7, 2022 ametoa wito wa kuimarisha ulinzi shirikishi katika maeneo yote ya Wilaya ya Geita ili kudhibiti vitendo vya wizi.
Mhe. Shimo akizungumza na wajumbe hao katika mkutano maalumu wa baraza la madiwani ulioketi katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya Nzera, kupokea taarifa ya fedha kiasi cha Bilioni 5 na milioni 340 kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 267 vya madarasa ya Sekondari, amesema kuwa licha ya kuimarisha ulinzi shirikishi ni vyema pia kuibua fursa za ujenzi wa vituo vya polisi kwenye maeneo yenye uhitaji wa haraka akitolea mfano wa eneo la Bukoli.
Aidha ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa namna inavyoendelea kufanya kazi zake huku akishauri kuongeza wigo wa kupata wazabuni kwa kanda, ili kuongeza ufanisi zaidi ya mwaka jana katika ujenzi wa madarasa ya UVIKO 19 ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Geita ilifanikiwa kukamilisha kwa ubora unaotakiwa jumla ya vyumba 354 vya madarasa.
Awali Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Adv. John Wanga akijibu hoja mbalimbali za wajumbe hao katika Mkutano huo amesema kuwa Halmashauri imeunda kamati mbalimbali za usimamizi kwa lengo la kufanikisha kufanya kazi nzuri huku akitoa wito wa kushirikiana badala ya kusuguana.
Adv. Wanga amesema kuwa wamejipanga kwa kuwatumia wazabuni wenye uwezo wa kuifanya kazi hiyo kwa wakati sahihi, huku akieleza kuwahusisha wataalamu katika kukagua ubora wa vifaa mbalimbali vitakavyotumika, wakiwemo TFS ambao watashiriki kukagua mbao zilizokomaa na zinazofaa kutumika.
Aidha ametoa wito kwa Madiwani hao ambao ndio wenyeviti wa WDC katika kata zao, kutoa taarifa kwa viongozi wa Halmashauri akiwemo yeye mwenyewe, pale wanapohitaji kuuliza kitu au kukutana na changamoto katika utekelezaji wa miradi hiyo huku akisisitiza kazi hiyo ya ujenziwa madarasa kufanyika kwa uwazi, uadilifu, na uwajibikaji.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa