Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Cornel Magembe ametoa wito kwa jamii, kuwawezesha wanawake katika sekta mbalimbali ikiwemo Kilimo ili kuwainua kiuchumi.
DC Magembe ametoa Wito huo kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani yaliyofanyika Kihalmashauri katika Kata ya Lwamgasa Wilayani Geita Machi 7, 2024.
Katika hotuba yake Magembe amesema kwenye maadhimisho hayo ameshuhudia wanawake waliowezeshwa kiuchumi na kwa sasa wanajitegemea kwa kuendesha kiwanda kidogo.
Amesema hata asasi za mikopo zikiwemo mabenki zinawahimiza wanawake kujiunga Pamoja na kuunda vikundi ambavyo vinaweza kuaminika na kupata mikopo.
Maandamano ya Wananchi mbalimbali waliojitokeza katika maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani yaliadhimishwa Kihalmashauri katika kata ya Lwamgasa Leo Machi 7, 2024.
Ametumia mhadhara huo, kuwahimiza wanawake kujiunga kwenye vikundi na kwamba mabenki yako tayari kuwakopesha wanawake.
“Tuwawezeshe wanawake kiuchumi, kwenye fursa mbalimbali za kilimo na kadhalika, tumeona pale wakati napita kwenye vikundi mbalimbali tumekuta kuna kikundi cha wanawake, kikundi kile kwasababu kimewezeshwa kimeweza kujenga Uchumi na leo kinajitegemea, leo mpaka wamefikia hatua ya kumiliki kiwanda kidogo” alisema DC Magembe.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Mhe. Khadija Said amemshukuru Mhe. Rais wa Jamahuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyowawezesha wanawake kushika nafasi mbalimbali za uongozi.
Amewataka pia wanawake kutumia vizuri siku ya wanawake Duniani kwa kuhakikisha wanafuatilia mienendo ya Watoto wao ili kujenga Taifa lililo bora.
“Mhe. Mgeni rasmi nichukue nafasi hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan, kwa jinsi alivyoweza kutupa nguvu kinamama wa Tanzania hii kuhakikisha kwamba tunashika nafasi mbalimbali, Lakini kuhakikisha kwamba anatutia ujasiriili tuweze kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi kuhakikisha kwamba tunaboresha familia zetu” alisema Makamu Mwenyekiti Geita DC Khadija.
Wanawake mbalimbali waliojitokeza katika uwanja wa Corona katika kata ya Lwamgasa kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani Leo Machi 7, 2024.
Katika maadhimisho hayo, Pamoja na mambo mengine Halmashauri ya Wilaya ya Geita imetoa misaada kwa makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuatambua jitihada za ziada kwenye uelimishaji jamii kuondokana na ukatili wa kijinsia.
Dkt Richard Buchadi Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita amesema imefika wakati kauli ya “mwanamke akiwezeshwa anaweza, iachwe na badala yake itambulike kwamba wanawake wanaweza hata bila kuwezeshwa”.
Kwenye Picha wakwanza kulia alieshika kidevu ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Dkt Richard Buchad, Katikati ni Mhe. Cornel Magembe Mkuu wa Wilaya ya Geita na WA kwanza kushoto ni Bi. Khadija Said Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, wakiwa kwenye maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani Leo Machi 7, 2024 yaliyofanyika Kihalmashauri katika kata ya Lwamgasa.
Dkt. Buchadi Amesema Rais Samia Suluhu Hassana amedhihirisha hilo kwa vitendo kutokana na kazi kubwa alizozifanya hapa nchini.
Aidha kauli mbiu ya siku ya wanawake mwaka huu 2024 ni “Wekeza kwa wanawake, kuharakisha Maendeleo ya Taifa na Ustawi wa Jamii”
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa