Na:Hendrick Msangi
MKUU wa Wilaya ya Geita Mhe Hashim Abdallah Komba amefanya ziara kata za Lwamgasa ikiwa ni sehemu ya kujitambulisha kwa wananchi Wilayani Geita pamoja na kusikiliza Kero za wananchi na kuzitafutia majibu katika kutekeleza maelekezo ya Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwatumikia wananchi kwa kuwafuata katika maeneo yao kusikiliza kero zao.
Akiwa kwenye Kata ya Lwamgasa Wilayani Geita, Mhe Mkuu wa wilaya aliweza kutembelea mradi wa shule ya msingi Majengo ambapo alikagua maboma ya madarasa yaliyojengwa kwa nguvu za wanachi kwa gharama ya Milioni 32 kwa kuchanga kila kaya kiasi cha shilingi 3000.
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe Hashim Abdallah Komba akipokea taarifa ya mradi wa shule ya msingi Majengo ambapo aliitaka uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita kuwaunga mkono wananchi katika ukamilishaji wa maboma yaliyo anzishwa kwa nguvu za wananchi ili kuchochea shughuli za maendeleo. Majengo hayo yamenjengwa kwa gharama ya shilingi milioni 32. Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji ilisema itamalizia maboma hayo kupitia fedha za CSR katika kuunga mkono juhudi za wananchi katika miradi ya maendeleo
Katika ukaguzi wa mradi huo, Mhe Komba aliiagiza ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita kuwaunga mkono wananchi ili kuchochea shughuli za maendeleo pamoja na kutengeza kanuni za kukwamua miradi viporo ili kuendelea kuwatia moyo wananchi pale wanapoanzisha maboma kwa nguvu zao.
Aidha Mhe Komba aliwataka watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita kujenga utamaduni wa kutumia vizuri fedha zinazoletwa na Mhe Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika utekelezaji wa miradi. “Fedha zinapokuja na maelekezo fanyeni tathmini kisha kuishauri serikali kwa kujenga hoja na kuzifanyia kazi muweze kumaliza miradi viporo kabla ya kuanza miradi mipya” alisema Mhe Komba.
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe Hashim Abdallah Komba akizungumza na wananchi wa kata ya Lwamgasa katika mkutano mkubwa wa hadhara ambapo aliwaeleza wananchi hao kuwa ndio wenye jukumu la kuijenga Halmashauri kwa kuwa tayari kuchangia mapato ya Halmashauri
Akiwa kwenye mkutano mkubwa wa hadhara kata ya Lwamgasa, Mhe Mkuu wa Wilaya alisikiliza kero mbalimbali za wananchi zikiwemo kero za fedha za kunusuru kaya masikini kupitia mfuko wa TASAF, mikopo ya vikundi vya ujasiriamali, milipuko kutoka mgodi ulio chini ya Kampuni ya uchimbaji wa Madini ya Dhahabu Buckreef Gold Limited inayosababisha mipasuko kwenye nyumba za wananchi ambapo wananchi hao waliulalamikia mgodi huo kutokutoa fidia, kero ya kutokusomewa mapato na matumizi.
Kero nyingine ambazo wananchi hao walimueleza Mkuu wa Wilaya ni pamoja na maafisa madini kutaka fedha ili kuweza kuwahudumia wachimbaji wadogowadogo, Ukosefu wa gari la kubeba wagonjwa kwenye kituo cha afya cha Lwamgasa, ukosefu wa mahakama na uwepo wa vibaka wanaopora mali za wananchi.
Wananchi wa Kata ya Lwamgasa wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe Hashim Abdallah Komba kwenye mkutano wa hadhara ambapo kero mbalimbali za wananchi hao zilipatiwa majibu. Aidha aliwapongeza wananchi wa Kata hiyo kwa namna wanavyojitolea kwenye miradi ya maendeleo
Akijibu kero hizo Mkuu wa Wilaya alitoa maagizo kwa watendaji wenye dhamana kutekeleza wajibu wa kuwatumikia wananchi kwa kushuka chini kwenda kuwasikiliza.
Pamoja na hayo Mhe Komba aliiagiza halmashauri kuendelea kutoa elimu juu ya namna wananchi wanavyotakiwa kujisajili kwenye vikundi ili kunufaika na mikopo ikiwa ni pamoja na kuweka majina kwenye mbao za matangazo kwenye ofisi za serikali za vijiji ya wanafaika wote wa mikopo inayotolewa na Halmashauri.
Aidha Mhe Komba aliwasihi wananchi hao kuendelea kumuunga mkono Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kumuombea na kuziunga mkono shughulizi zote za maendeleo ikiwa ni pamoja na kuchangia mapato ya Halmashauri. “Kila mmoja ajenge utamaduni wa kuchangia pato la taifa,mjenga nchi ni mwananchi na mbomoa nchi ni mwananchi mwenyewe,” alisema Mhe Komba.
Pamoja na hayo aliwataka wananchi kuendelea kushiriki kikamilifu katika maswala ya ulinzi na usalama kwa kutoa ushirikiano kwenye vyombo vya usalama pale wanapoona matendo ya kiuhalifu na kuwasihi kutokujichukulia sheria mkononi. Pia aliwataka wananchi hao kuzingatia maswala ya usafi wa mazingira katika maeneo yao ili kuendelea kuwa na afya njema.
Mh. Kaparatus Joseph Sasembe diwani wa kata ya Lwamgasa akimshukuru Mhe Mkuu wa Wilaya kwa kufanya zaira kwenye kata hiyo ambayo wananchi walimpokea kwa shangwe na kufurahia ujio wake katika kusikiliza na kutatua kero za wanachi.
Mwisho Mkuu huyo wa Wilaya aliwaomba wananchi kuendelea kumpa ushirikiano ili kuendelea kuwahudumia na kuwataka watumishi wote wa halmashauri kujenga utamaduni wa kuwa na uvumilivu kuwasikiliza wananchi na sio kuwapuuza na pale wananchi wanapotoa taarifa zifanyiwe kazi ikiwa ni pamoja na kuwafuata wananchi kwenye maeneo ya kusikiliza kero zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa