Na: Hendrick Msangi
WATUMISHI wa umma wasio waadilifu wamepewa onyo kali juu ya matumizi ya Fedha za miradi ya Maendeleo zinazoletwa kwenye maeneo yao.
Akizungumza katika Ziara ya kukagua Miradi ya Maendeleo ndani ya Kata ya Nyarugusu Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Mhe Hashim Abdallah Komba amekemea vikali tabia ya Watumishi wa umma ambao hawatimizi wajibu wao kusimamia Miradi ya Maendeleo.
Aidha ameiagiza Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita kuweka utaratibu wa kukamilisha Miradi iliyo anzishwa kwa nguvu za Wananchi ili kuendelea kuwapa hamasa Wananchi katika Miradi ya Maendeleo.
Katika Ziara hiyo, Mhe Komba ametembelea Miradi ya Maendeleo katika Vijiji vya kata hiyo ambavyo ni Nyarugusu, Ililika, Mawemeru na Kijiji cha Mwabageni ambapo amekagua Miradi ya ujenzi wa zahanati, nyumba za Watumishi na ujenzi wa Shule katika kata hiyo ya Nyarugusu yenye utajiri wa Madini.
Mhe. Hashim Abdallah Komba Mkuu wa Wilaya ya Geita akishirikiana nawananchi wa kata ya Nyarugusu kuchimba msingi kwenye ujenzi wa be Bweni la Wasichana shule ya Sekondari Evarist ambalo lina uwezo wa kubeba wanafunzi 80. Serikali kupitia mfuko wa kunusuru kaya masikini (TASAF) imetoka kiasi cha Shilingi milioni 180 na Wananchi watachangia asiliamia 10 katika ujenzi huo.
Mhe Komba, .amempongeza Diwani wa Kata hiyo Mhe Salehe Juma Msene kwa namna anavyopambana kusukuma Miradi ya Maendeleo katika kata hiyo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita ndg Karia Rajabu Magaro amesema Serikali inatambua juhudi wanazozifanya Wananchi katika ujenzi wa Miradi mbalimbali ya Maendeleo na tayari Halmashauri imepeleka orodha ya Miradi ambayo haijakamilika TAMISEMI kwa ajili ya kuratibiwa ili iweze kukamilika na iwanufaishe wananchi.
Pamoja na hayo Ndugu Karia amesema amewaelekeza Wahandisi wa Halmashauri kupita katika kila mradi ili kufanya tathmini ya ukamilishwaji ili kuweza kuwatumia wadau wa Maendeleo katika ukamilishaji wa Miradi hiyo.
Ndg Karia Rajabu Magaro Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita akishirikiana na Wananchi wa kata ya Nyarugusu kuchimba msingi kwenye ujenzi wa Bweni la Wasichana shule ya Sekondari Evarist ambalo lina uwezo wa kubeba wanafunzi 80. Serikali kupitia mfuko wa kunusuru kaya masikini (TASAF) imetoka kiasi cha Shilingi milioni 180 na Wananchi watachangia asiliamia 10 katika ujenzi huo.
Akijibu Kero za Wananchi, Mhe Komba amekemea tabia za rushwa zinazofanywa na Watumishi wa umma baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi wakilalamikia baadhi ya Watumishi wa Kituo cha Afya Nyarugusu kuomba rushwa kwa wagonjwa wanaoenda kupata matibabu ambapo ameiagiza Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) Wilayani Geita kichunguza tuhuma hizo ili Wananchi hao wapate huduma bora.
Wananchi wa kata ya Nyarugusu wakifuatilia Mkutano wa hadhara wa Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Hashim Abdallah Komba alipotembelea kata hiyo kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za Wananchi.
Mkuu huyo wa Wilaya ameendelea kuwasisitiza Watumishi wa umma kushuka chini kusikiliza kero za Wananchi. " Tukishindwa kusimamia kero za Wananchi tutazalisha uvunjifu wa amani" amesema Mhe Komba.
Aidha ameitaka Halmashauri ya Kijiji kutoa taarifa kwa Wananchi juu ya fedha zinazoletwa kwenye maeneo yao kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ili wafahamu na kuendelea kuwa na imani na Serikali yao inayo ongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa