Na: Hendrick Msangi
MKUU wa Wilaya ya Geita Mhe Hashim Abdallah Komba, ameanza operesheni kukagua Miradi ya Maendeleo Wilayani Geita May 15 ambapo operesheni hiyo itamalizika kwa awamu ya kwanza May 23 2024 kwa Kata 9 ndani ya Halmashauri ya wilaya ya Geita.
Wananchi wa Kata ya Bukoli wakifuatilia Mkutano wa Hadhara wa Mkuu wa Wilaya ambapo walitoa kero zao ikiwa ni pamoja na kero ya ukosefu wa miundombinu ya Umeme, miundombinu mibovu ya barabara, uhaba wa walimu wa Kike kwenye shule za kata hiyo.
Akiwa kwenye kata ya Bukoli yenye Jumla ya Vijiji 4, ambavyo ni Ntono, Ikina, Bugogo na Bujula, Mhe Komba amekagua miradi ya Maendeleo na kutoa maelekezo kwa wasimamizi wa Miradi hiyo katika ukamilishwaji.
Awali alimkaribisha Mkuu wa Wilaya katika kata ya Bukoli, Mhe Faraj Seif Diwani wa Kata ya Bukoli, amesema kuchelewa kwa Miradi mingi katika kata hiyo kunatokana na Kampuni ya madini (GGML) kuchelewesha vifaa kwenye miradi ikiwa ni pamoja na kutokutoa taarifa ya mradi na mafundi kufika site bila uongozi wa wasimamizi wa mradi kufahamu .
Miradi ya Maendeleo ambayo Mhe Mkuu wa Wilaya ameitembelea ni pamoja na ujenzi wa zahanati kijiji cha Ikina kinachojengwa kwa nguvu za Wananchi na kufika usawa wa madirisha ambapo alipokea taarifa ya ujenzi wa kituo hicho.
Katika kuunga jitahada za nguvu za Wananchi, Mkuu wa Wilaya aliongoza harambee ndogo iliyopelekea kupata zaidi ya mifuko 150 ya saruji.
Ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Ikina Kata ya Bukoli inayojengwa na nguvu za Wananchi. Katika Ziara ya kukagua Miradi hiyo Mhe Komba ameongoza harambee ndogo iliyopelekea kupatikana kwa mifumo ya saruji 150.
Mradi mwingine ambao Mhe Komba ameutembelea ni Kituo cha Afya Ntono Na ujenzi wa nyumba ya mtumishi mbili kwa moja ambayo ipo hatua za ukamilishwaji.
Aidha Mhe Komba aliweza tembelea mradi wa Kituo cha Afya Kijiji cha Bugogo na kupokea taarifa ya ujenzi wa jengo la mama na mtoto na jengo la upasuaji ambapo alipongeza ujenzi wa mradi huo na kuiagiza ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Geita kuweka bajeti kukakimilisha ujenzi huo.
Aidha amewataka Watumishi aliombatana nao kutoka Halmashauri ya wilaya ya Geita kuwasaidia wananchi kuanzisha Miradi yenye vipaumbele.
" Nitoe Rai kwenu kuwasaidia wananchi kuibua Miradi ambayo itakuwa na vipaumbele ili kuendelea kuinga mkono Serikali" amesema Mhe Komba.
Pamoja na hayo Mhe Komba ameagiza Wahandisi kutembelea Miradi na kubainisha mapungufu yaliyopo ili kuwapa GGML ambayo wanaitekeleza miradi hiyo kupitia CSR kufanya marekebisho sehemu zilizo na kasoro.
Mhe Komba akipokea taarifa ya ujenzi wa Miradi Kata ya Bukoli ambapo amesema kuchelewa kwa ukamilishwaji wa Miradi viporo ni Jambo ambalo halikubaliki kwani Miradi ya CSR sio ya hisani bali ni wajibu wa wamiliki wa migodi kujenga utamaduni wa kurudisha kwenye jamii.
Pamoja na kukagua Miradi hiyo, Mhe Komba amefanya Mkutano wa Hadhara katika kata hiyo ikiwa ni sehemu ya maagizo ya Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushuka chini na kuwasikiliza Wananchi.
Alimkaribisha Mkuu wa Wilaya katika Mkutano wa Hadhara kusikiliza kero za Wananchi, Diwani wa Kata ya Bukoli Mhe Faraj Seif amesema ameshirikiana na wananchi wote wa Vijiji vinne katika Kutekeleza Miradi ya kimkakati katika kata hiyo pamoja na uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Geita.
Akizungumza katika Mkutano huo wa kusikiliza na kutatua kero za Wananchi, Mhe Komba amewataka Wananchi hao kuendelea kudumisha ulinzi na Usalama kwa kuendelea kuilinda amani na utulivu kwenye maeneo yao kwa kukemea matendo ya kihalifu.
Mhe Komba ameendelea kwa kuwataka Watumishi wa umma kuendelea kushuka chini kusikiliza kero za Wananchi katika nafasi walizopewa na kuwataka kuwa na dawati la malalamiko katika Vijiji ili kusikiliza kero za Wananchi.
Akijibu Kero ya Upungufu wa walimu wa masomo ya Sayansi, Mhe Komba ameiagiza Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji kuweka mpango wa kuwekeza katika mfuko wa Elimu kupitia CSR na mapato ya ndani.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Geita ndg Karia Rajabu Magaro amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan inaleta fedha nyingi za miradi hivyo amewataka Wananchi hao ambao wanasimamia Kamati za ujenzi wa Miradi mbalimbali kuwajibika ipasavyo.
Ujenzi wa jengo la mama na mtoto na jengo la upasuaji kituo cha afya Bukoli Kijiji cha Bugogo uliojengwa kwa thamani ya Shilingi milioni 200. Mradi huo unakadiriwa kugharimu kiasi cha Shilingi 291,000,000 hadi kukamilika.
" Nawaomba mkazitumie kamati zenu kwenye vijiji husika kwa kuwa bega kwa bega Kutekeleza majukumu yenu ili Miradi ikamilishwe kulingana na thamani inayotakiwa." amesema Magaro.
Ziara hiyo itaendelea kwa kata nyingine katika awamu ya kwanza ambazo ni Butobela, Bujula, Nyamalimbe, Kamena, Nyalwanzaja, Nyaruyeye, Nyarugusu na kumalizia kata ya Nyakamwaga.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa