Na: Hendrick Msangi
NYAMALIMBE MAY 18, 2024
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe Hashim Abdallah Komba ameendelea na ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi katika Halmashauri ya wilaya ya Geita May 18 katika kata ya Nyamalimbe inayoongozwa na Mhe Jeremia Ikangaa diwani wa kata hiyo.
Katika ziara hiyo, Mhe Komba ameendelea kuwasisitiza watumishi wa umma kuendelea kusimamia vizuri matumizi ya fedha za serikali zinazopelekwa katika maeneo yao huku akiwataka kushuka chini kuwasikiliza wananchi na kutatua changamoto zinazowakabili kupitia madawati yanayotembea.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Geita Nicolaus Kasendamila akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe Hashim Abdallah Komba, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita ndg Karia Rajabu Magaro katika Ziara ya Kukagua Miradi ya Maendeleo kata ya Nyamalimbe.
Pamoja na hayo Mhe Komba amewataka wananachi kuendelea kudumisha ulinzi na usalama katika maeneo yao kwa kuwataka kuwa mabalozi wazuri katika maeneo yao kwa kutoa taarifa juu ya vitendo vya kiuhalifu na kuwasisitiza kuendelea kujitolea kwenye shughuli za maendeleo.
Akiwa kata ya Nyamalimbe, Mhe Komba amefanya ukaguzi wa miradi katika kijiji cha Nyamalimbe, Buzanaki, Lwamizo na Nyamigogo ambapo amekagua miradi ya afya ikiwepo ujenzi wa jengo la mama na mtoto lililojengwa kwa nguvu za wananchi kwa kiasi cha Shilingi 9,000,000 na wadau wengine wa maendeleo huku CSR wakiwezesha vifaa vya kuezeka na kulipa mafundi.
Mhe Hashim Abdallah Komba akiwa katika Ziara ya kukagua Miradi ya Maendeleo kata ya Nyamalimbe ambapo amewataka Wananchi kuendelea kijitokeza kuwa mstari wa mbele katika kazi za kujitolea ili kuchochea maendeleo kwani serikali inaendelea kuunga juhudi zao katika kukamilisha miradi ya maendeleo.
Aidha katika kijiji hicho Mh Komba ametembelea nyumba ya mtumishi wa zahanati lilioanzishwa kwa nguvu za wananchi shilingi 8,000,000 na kupata fedha nyingine kutoka kwa Mh Mbunge wa Jimbo la Busanda Mhandisi Tumaini Magesa kiasi cha shilingi 14,000,000.
Miradi mingine aliyoikagua ni pamoja na Ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Lwamizo , ujenzi wa nyumba ya mtumishi wa zahanati , na kwa upande wa kijiji cha Buzanaki amekagua ujenzi wa jengo la zahanati na nyumba ya mtumishi zilizo jengwa kwa nguvu za wananchi pamoja na CSR na mapato ya ndani ya Halmashauri.
Mhe Komba amewataka wananchi kuendelea kijitokeza kuwa mstari wa mbele katika kazi za kujitolea ili kuchochea maendeleo kwani serikali inaendelea kuunga juhudi zao katika kukamilisha miradi ya maendeleo.
Wakati huo huo ameitaka ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji kupitia idara ya mipango kuwaongoza wananchi katika kuibua miradi itakayoendana na vipaumbele vya Serikali ili iweze kupata msukumo na kuikamilisha kuliko kuibua miradi mingi isiyokamilika.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Karia Rajabu Magaro amesema Halmashauri itaendelea kushirikiana na Mhe Diwani wa kata hiyo kuipa kipaumbele miradi iliyo anzishwa kwa nguvu za wananchi kulingana na bajeti za Halmashauri.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa