Na: Hendrick Msangi
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe Hashim Abdallah Komba amefanya ziara ya kujitambulisha katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita pamoja na kuzungumza na watumishi wa Halmashauri.
Mkuu huyo wa Wilaya amefanya ziara hiyo ikiwa ni mara yake ya kwanza kuzungumza na watumishi wa Halmashauri kufuatia mabadiliko yaliyofanywa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Machi 09, 2024 ambapo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe Cornel L.B. Magembe alihamishiwa Wilaya ya Sikonge Mkoani Tabora huku Mhe Hashim Abdallah Komba akihamishiwa Wilaya ya Geita akitokea Wilaya ya Ubungo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita ndugu Karia Rajabu Magaro amesema watumishi hao watazingatia na kufuata maelekezo yote aliyoelekeza Mkuu wa wilaya Mhe Komba
Awali akimkaribisha kuzungumza na watumishi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita ndugu Karia Rajabu Magaro alisema Halmashauri ya Wilaya ya Geita ina jumla ya watumishi 5218 na kwa upande wa miradi Halmashauri katika kipindi cha miaka mitatu (2021/2022. 2022/2023 na 2023/2024) imetekeleza miradi yenye jumla ya shilingi 38,932,247,774.25 kutokana na fedha za mapato ya ndani, ruzuku ya serikali kuu pamajo na wa wadau wa maendeleo.
Aidha Karia alisema Halmashauri kwa mwaka 2023/2024 ililenga kukusanya shilingi 5,135,900,000 na imefanikiwa kukusanya shilingi 6,272,030,392.95 sawa na asilimia 112.25 ambapo kwa mwaka 2023/2024 Halmashauri imelenga kukusanya shilingi 6,774,614,000.00
Akizungumza na watumishi katika Kikao Kazi hicho, Mhe Komba alisisitiza swala la nidhamu na upendo kwa watumishi wa umma ikiwa ni pamoja na kuheshimiana pasipo kujali vyeo na nafasi walizo nazo.
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe Hashim Abdallah Komba akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Machi 18, 2024 alipofanya kikao kazi na watumishi hao ambapo aliwataka kutuwa Wabunifu kwa kuwa na mawazo mbadala nje ya majukumu yao ya kila siku.
Aidha Mhe Komba alieleza mambo ambayo angependa watumishi hao kuyafahamu ili kuweza kufanya kazi kwa weledi kuwa ni kuzingatia swala la muda, kuwa wa wazi katika utendaji wao kuepusha migogoro na kujiepusha na majungu ambayo huondoa ufanisi katika kazi. “Tuwaze kuwa wabunifu na kuwahudumia wananchi, tunataka watu wafanye kazi” alisema Mhe Komba.
Pamoja na hayo aliitaka timu ya menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya kuwa na institutional ownership mechanism, akimaanisha kila mmoja kuimiliki Taasisi ili kuwa na uwelewa mmoja wa shughuli zote za Halmashauri. “Natamani tubebeane mapungufu tusisemeane mapungufu tufanye kazi kwa ushirikiano kuwa na umoja, kupeana taarifa na mrejesho wa kazi ambazo tumepena maana jambo likiharibika linaharibika kwa watu wote” Alisisitiza Mhe Mkuu wa Wilaya.
Akiendelea kuzungumza katika kikao kazi hicho na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Mhe Mkuu huyo wa Wilaya alieleza vipaumbele ambavyo angependa watumishi hao wavifahamu ni swala la Mapato na Miradi ya maendeleo ambapo alisisitiza ukusanyaji wa mapato kwa kila chanzo ili kufikia lengo lililowekwa , kuwa na mfumo wa ukusanyaji wa madeni na kusisitiza kile kinachokusanywa kiache alama kwa kufanya miradi ya maendeleo. “Tuachane na visababu tuwe watumishi tunaotaka matokeo, nataka miradi ya maendeleo kuanza kwa wakati na kukamilika kwa wakati” alisema DC Komba.
Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe Hashim Abdallah Komba wakati wa kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita. Watumishi hao wametakiwa kutoka kwenye maofisi kwenda kusikiliza kero za wananchi.
Akiendelea kuvitaja vipaumbele vyake, Mhe Komba aliutaka uongozi wa halmashauri kutatua kero za watumishi na wananchi kwa kujenga utamaduni wa kuwasikiliza kwa kuwaheshimu watu wote wanaofika kupata huduma kwa nafasi zao pasipo kuwadharau na kuwataka kutoka kwenye ofisi kwenda kusikiliza kero za wananchi.
Pamoja na vipaumbele hivyo, alisisitiza swala la ulinzi na usalama akiwataka watumishi hao kutokuzipuuza hisia za wananchi pale wanapukuwa na manung’uniko na kuwataka kutoa taarifa zote zinazopelekea viashiria vya uvunjifu wa amani,
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe Hashim Abdallah Komba akiwa ndani ya ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Ndugu Karia Rajabu Magaro alipotembelea Halmashauri ya Wilaya Machi 18.2024 ambapo alizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Mwisho Mkuu wa Wilaya aliwataka watumishi kuwa wabunifu kwa kuwa na mawazo mbadala nje ya majukumu yao ya kila siku ili kuweka alama (Extra ordinary Perfomance) kwenye utendaji kazi wao wa kila siku.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa