Wananchi wa Kata ya Senga Halmashauri ya Wilaya ya Geita wamemuomba Mkuu wa Wilaya Mhe Hashim Komba kuwasaidia kupata kituo cha afya katika kata hiyo ili kupunguza umbali mrefu wanaotumia kutoka kwenye kata hiyo kufuata huduma katika maeneo mengine.
Hayo yamesemwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Buligi kata ya Senga Julai 30, 2024 wakati wa ziara ya Mhe Komba alipotembelea kukagua miradi ya maendeleo katika vijiji vya Chanika,Kaseni, Lwenazi na Buligi.
Ujenzi wa jengo la Zahanati kijiji cha Chanika ambao umejengwa kwa nguvu za wananchi hadi hatua ya boma. Mradi huo utakapokamilika utapunguza umbali wa zaidi ya Kilimeta 7 kwenda kijiji cha Senga kupata huduma. Mkuu wa Wilaya ameiagiza ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji kuweka kwenye bajeti za CSR na mapato ya ndani ili kukamilisha mradi huo uanze kutumika.
Naye Diwani wa Kata ya Senga Mhe Edward Tumbo, ameomba miradi ya zahanati iliyoko katika vijiji vya Chanika, Kaseni na Buligi katika kata hiyo ikamilike ili kuendelea kupunguza umbali mrefu wa wananchi kufuata huduma katika kata za jirani.
Ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Kaseni uliojengwa kwa nguvu za wananchi, mfuko wa jimbo na mapato ya ndani wenye thamani ya shilingi milioni 14.8 ukiwa katika hatua ya boma.
Akizungumza katika Mkutano huo, Mhe Komba amewataka wananchi hao kuwa na ndoto za kuwa na kituo cha afya kwa sababu kituo cha afya kitawasaidia watu wengi wakati ukamilishwaji wa zahanati katika vijiji ukiendelea kwa kupitia mapitio ya bajeti za halmashauri.
Mradi wa vyumba 6 vya madarasa shule ya sekondari Lwenazi ulionza kwa nguvu za wananchi na kupokea fedha za ukamilishwaji kupitia mfuko wa SEQUIP kiasi cha shilingi milioni 75.
Aidha Mhe Komba ametoa rai kwa watumishi wa umma kuwahudumia wananchi kwa unyenyekevu na upendo kila mmoja kwenye eneo lake analotolea huduma ikiwa ni pamoja na kuwa na madawati ya kusikiliza kero za wananchi.
Kuhusu wanufaika wa kaya masikini Mkuu wa Wilaya amewaagiza waratibu wanaosimamia mfuko wa kuwezesha kaya maskini (TASAF) kutoa elimu kwa jamii juu ya namna sahihi ya utolewaji wa fedha hizo ili kuepusha migogoro kati ya wananchi na serikali yao na kuwataka wanufaika wa fedha hizo kuzitumia vile inavyostahili.
”Toeni elimu kwa wananachi ili wale ambao wanastaili wawekwe bayana ili kuepuka migogoro kati ya wananachi na serikali yao” amesema Mh Komba.
Mradi wa Ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Buligi kata ya Senga. Zahanati hiyo imejengwa kwa nguvu za wananchi, mfuko wa jimbo, ofisi ya mkuu wa wilaya, Halmashauri na Mgodi wa dhahabu kupitia mfuko wa CSR kutoa vifaa vya kuezeka. Jumla ya shilingi milioni 31,734,400.
Vilevile ameiagiza Idara ya maendeleo ya jamii kuwatangazia wananchi pindi dirisha la mkopo linapofunguliwa ili wananachi wapate elimu juu ya mikopo isiyokuwa na riba inayotolewa na serikali na kuepukana na mikopo inayowaumiza maarufu kama kausha damu.
Kwa upande mwingine Mhe. Komba amewasisitiza wakazi wa Kata ya Senga kujitokeza kwa wingi pindi zoezi la uboreshaji wa daftari la mpiga kura litakapo anza Agosti 5, 2024 ili kuboresha taarifa zao kwa lengo la kijiandaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 pamoja na uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba,2024.
Pamoja na hayo Mhe.Komba amewasisitiza wakazi wa kata ya Senga kusimamia vema ulinzi na usalama katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na kukataa vitendo vya uporaji, ubomoaji wa maduka na makazi pamoja na kuwataka wananachi kutoa taarifa katika vyombo vya dola kwa wale wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu.
’’Nitoe rai kwenu wana Senga kupitia kijiji hiki cha Buligi lindeni amani na utulivu wa Taifa la letu’’. Amesisitiza Mhe Komba.
Wananchi wa Kata ya Senga wakifuatilia Mkutano wa Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe Hashim Komba alipotembelea kata hiyo kukagua miradi ya maendeleo
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa