Na: Hendrick Msangi.
Mkuu wa Wilaya ya Geita , Mh Cornel Magembe amefanya ziara katika kijiji cha Mkolani kata ya Kamuhanga septemba 18, 2023 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inavyoeleza katika kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu.
Maghembe katika ziara yake ambayo aliambatana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya, wakuu wa Divisheni mbalimbali za halmashauri ya wilaya ya Geita, Diwani kata ya Kamuhanga, Diwani viti maalum, Mwenyekiti wa Kijiji pamoja na mtendaji wa kijiji aliweza kusikiliza kero za wananchi wa Kata hiyo na kuzitolea ufafanuzi.
Awali akimkaribisha katika Kata hiyo,Diwani wa Kata ya Kamuhanga ndugu Joseph Juma alimueleza Mkuu wa wilaya kero kubwa kwa wananchi wa kata yake ni ubovu wa barabara ya Geita –Isamilo-Busekelo yenye urefu wa kilometa 20.
Kwa mujibu wa Diwani huyo barabara hiyo imekuwa ikitolewa ahadi nyingi kwa nyakati tofauti na viongozi waliotangulia na Mbunge ambapo mpaka sasa hakuna majibu.Akiendelea kueleza kero za wananchi kwa Mkuu wa wilaya, Diwani Joseph alimueleza mkuu wa wilaya kuwa ipo zahanati ambayo imekuwa ikiwasaidia wanachi lakini haina umeme ambapo wamama wanajifungulia katika mazingira magumu jambo ambalo sio salama,
“Zahanati ina sola lakini msimu wa mvua zinakosa nguvu hivyo kukosa umeme wa uhakika” alifafanua Diwani.
Kero nyingine ambayo Diwani Joseph alimueleza Mkuu wa Wilaya ni changamoto ya maji safi na salama , ukosefu wa walimu wa kike kwenye baadhi ya shule inayopelekea watoto wa kike kutaabika pindi wanapohitaji msaada.
Pamoja na diwani kutoa baadhi ya kero kutoka kwa wananchi, Mkuu wa wilaya Mh Magembe aliwakaribisha wananchi hao ili kueleza kero zao ambazo diwani wao hakuzitaja,Baadhi ya wananchi walio jitokeza kumueleza mkuu wa wilaya kero zao, walisema wanaomba kujengewa kituo cha polisi ili kukabiliana na matukio ya kiuhalifu katika kata yao, kusomewa mapato na matumizi ya kata yao, bei kubwa ya mbegu za mahindi ambapo wananchi wanashindwa kumudu gharama.
Wakiendelea kutoa kero zao mbele ya Mkuu wa wilaya, wanachi hao walisemema kumekuwa na usumbufu wa kupata matibabu hasa wakati wa siku za mwisho wa wiki, ikiwa ni pamoja na jengo la zahanati kuchukua muda mrefu kukamilika, pia TANESCO kushindwa kupeleka umeme kwenye zahanati ya Kamuhanga.
Aidha wananchi hao walimueleza Mkuu wa wilaya ,kuchangishwa fedha kwa ajili ya kuwalipa walimu ambao wanajitolea kufundisha wanafunzi, ambapo walisema ni gharama kwao kuanza kuchangishwa fedha na kuitaka serikali kuliona hilo.
Akijibu maswali hayo yaliyowasilishwa na diwani pamoja na wananchi, Mh Magembe aliunga mkono wazo la wakazi wa kijiji cha Mkolani kilicho kata ya Kamuhanga kutaka kuanzishwa Kituo kidogo cha polisi katika eneo hilo ili kukabiliana na matukio ya uhalifu na ukatili wa kijinsia na kulinda mali na usalama wa raia.
Maghembe alisema kituo cha polisi kipo kata ya jirani , kwa sababu ya ufinyu wa bajeti ndio maana hakujajengwa vituo vya polisi kila kata hivyo alimtaka diwani kukaa na kamati yake na kuona namna ya kuanza mchakato wa kuwa na kituo kidogo cha polisi.
Akiendelea kujibu maswali ya wanachi walio jitokeza katika mkutano huo , Mh Magembe aliwataka wakazi wa kijiji hicho kujitokeza kwenye vikao vinavyoitishwa na serikali ya kijiji ili kupata taarifa za mapato na matumizi ya kijiji kila baada ya miezi mitatu.
“Jitokezeni katika mikutano hiyo kujua kama kuna fedha iliyo ingia kijijini au hakuna kwani ni muhimu sana katika maendeleo ya kijiji na serikali kwa ujumla,” alisema.
Kuhusu swala la mbolea ya ruzuku , Mh Mkuu wa wilaya aliwapongeza wananchi kwa kufanya kilimo na kuitikia vyema wito wa matumizi ya mbolea ya ruzuku inayotelewa na serikali .
Naye Mkuu wa Divisheni ya Kilimo kutoka Halmashauri ya wilaya hiyo Dk Alphonce Bagambabyaki aliwaeleza wananchi hao kuwa Chama cha Ushirika tayari kina mbolea na kwa mawakala wote .
Mbolea ni ya ruzuku hivyo wananchi waende kwa mawakala kupata mbolea kwani Serikali imeshatoa mbolea ipo kwenye vyama vya ushirika na mawakala wananchi waweze kuipata kwa urahisi , na kuhusu bei za mahindi zipo kawaida kwani mahindi hayana ruzuku alisema Dokta Bagambabyaki akimuwakilisha Mkurugenzi wa Halmashauri hiyoNaye Mganga mkuu wa Wilaya Dk Modest Buchri akijibu swali la zahanati kutokutoa huduma stahiki siku za mwisho wa wiki, alisema jambo hilo amepata taarifa na aliwataka radhi wananchi na kuahidi kulifanyia kazi.
Mh Magembe aliwa ahidi wananchi hao kupata huduma ya umeme kwenye zahanati ya Kamuhanga kwani kunahitajika nguzo nane ambazo zitapatikana wakati mkandarasi atakapo anza kufanya kazi ya kusambaza umeme.
Naye Mkuu wa Divisheni ya Mipango katika halmashauri hiyo Bi Sarah Yohana alisema Mgodi wa Geita (GGML) kila mwaka wanatoa bilioni 9 ambapo kwa kata ya Kamuhanga zitapelekwa Milioni 70 kwa ajili ya miradi inayotekelezwa na serikali Akimalizia kujibu maswali ya wanachi hao ambao walikuwa na kiu na shauku ya kujua ujio wa Mkuu wa wilaya Mh Cornel Magembe utakuwa na majibu gani ya kero ambazo zimechukua muda mrefu , Mh Magembe aliwaeleza wananchi hao swala la elimu ni la msingi kwa maendeleo ya taifa, na kwa kuwa uhitaji wa walimu ni mkubwa na bado katika kata yao haijapata walimu wa kutosha ni wajibu wa wanachi kuchangia gharama za kuwalipa walimu wa muda mfupi katika shule zao ila kuwepo na utaratibu mzuri wa ukusanyaji wa michango hiyo kwa kuandaa muhtasari ambao utasainiwa na Mkuu wa Wilaya kabla ya zoezi hilo kuanza.
Aidha aliwataka walimu kutokuwaadhibu watoto na kuwarudisha nyumbani kwa kushindwa kuchangia gharama hizo bali serikali ya kijiji ndio ichukue hatua madhubuti kwa wazazi wao.
Maghembe aliwashukuru wananchi wa Kata ya Kamuhanga kwa kujitokeza katika mkutano na kuwataka kuendelea kuitunza Amani ya nchi yao na kuendelea kuiombea.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa