Wahudumu wa Afya na Lishe Wilayani Geita, wamehimizwa kutoa elimu sahihi juu ya umuhimu wa chanjo kwa watoto, ili kuondokana na tatizo la magonjwa nyemelezi pindi mtoto akiwa katika hatua za ukuaji.
Akizungumza hapo jana kwenye Kikao cha tathmini ya taarifa ya utekelezaji wa shughuli za lishe Octoba-Disemba 2024, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Geita, Katibu Tawala Bi Lucy Beda amesema kuwa ni muhimu kwa akina mama kupewa elimu ya kutosha juu ya Utoaji wa Chanjo kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano.
"Lazima akina mama wapewe elimu juu ya umuhimu wa kuwapa watoto chanjo. Hii itasaidia kupunguza vifo miongoni mwa wawoto pamoja na kuwa na usatwi kwenye jamii yetu." Amesema Bi. Lucy Beda.
Katibu Tawala Bi Lucy Beda akihudhuria zoezi la upimaji wa presha kwa hiari lililoratibiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Geita, kabla ya kuanza kwa Kikao cha Tathmini ya utekelezaji wa shughuli za Lishe, Octoba-Disemba katika ukumbi wa EPZ, Bombambili.
Aidha, Bi. Beda aligusia pia kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa Marbug nchini, ambapo ameagiza elimu iendelee kwa usahihi maeneo ya magereza, mashuleni, pamoja na maeneo yenye mikusanyiko ya watu kama Katoro na Nkome, huku akizitaka Halmashauri ziratibu vikao vya afya kwa wakati.
Kwa upande mwingine, Afisa Lishe kutoka Halmashauri ya Wilaya, Geita, Bi. Nasim Ginga amesema kuwa, katika kipindi cha robo ya pili, Oktoba-Disemba, jumla ya watoto 14,361 Kati ya 15,381 chini ya mwaka mmoja, sawa na 93%, wameweza kupatiwa chanjo.
Afisa Lishe kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Bi Nasim Ginga amesema kuwa kwa mwaka 2024, Halmashauri ilifanikiwa kutoa chanjo kwa watoto 59,735 kati ya 61,528 chini ya mwaka mmoja, sawa na 97%.
Miongoni mwa mikakati ambayo ipo kwaajili ya kuinua kiwango cha utoaji wa chanjo kwa kipindi cha Januari-Machi 2025, ni pamoja na kuendelea kushirikiana na viongozi ngazi ya vijiji na mitaa kutoa elimu juu ya umuhimu wa chanjo kwa jamii, huku pia kukiwa na lengo la kuimarisha utoaji wa chanjo kwa njia ya huduma za mkoba katika maeneo magumu kufikika kama visiwa na machimbo madogo kupitia Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi, na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM).
Baadhi ya Wajumbe wa Kikao cha Tathmini ya utekelezaji wa shughuli za Lishe, wakifuatilia mada mbalimbali.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa