Mkuu wa Wilaya ya Geita Mheshimiwa Wilson Shimo amelitaka baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita kuielimisha na kuihamasisha jamii kupanda Miti kwa wingi ikiwa ni hatua ya kukabiliana na Ongezeko la joto linalosababishwa na uharibifu wa Mazingira .
Ametoa kauli hiyo Novemba 12, 2021 wakati akihutubia baraza hilo katika siku ya kufunga Mkutano wa kawaida wa Baraza la Madiwani wa robo ya kwanza kwa mwaka wa fedha 2021/2022, uliokuwa ukijadili taarifa za kamati za kudumu za Halmashauri kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba, 2021.
Mheshimiwa Shimo amesema kuwa kumekuwa na mabadiliko makubwa ya hali ya hewa ikiwemo ongezeko kubwa la joto duniani, hivyo amewataka Waheshimiwa Madiwani kuwahamasisha wananchi kupanda miti kwa wingi nyumbani, maeneo tengefu na hata kuanzisha mashamba ya miti ili kukabiliana na hali hiyo.
Wakati huo huo amewataka pia kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi kulima mazao ya chakula na biashara yasiyohitaji mvua nyingi sana, kwa kuwa msimu huu unatazamiwa kuwa na mvua chache.
Ameendelea kusema kuwa awali amefanya ziara katika Maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Geita akiwa na wataalamu wa zao la pamba, ili kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi kulima zao hilo msimu huu.
Awali akijibu maswali kutoka kwa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Afisa kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Richard Kapyela, alisema kuwa serikali imekuja na utaratibu mzuri wa kuwakopesha wakulima wa zao la pamba mbegu badala ya kununua, huku akiwataka kulima zao hilo kwa wingi kuanzia Novemba 15 hadi Decemba 15 mwaka huu kwa kuwa hali ya hewa ya msimu huu inaruhusu.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa