Nzera-Geita
Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Geita leo Februari 4,2026 limekutana katika Mkutano wake wa Kawaida wa robo ya pili ambapo taarifa za utekelezaji wa shughuli za maendeleo ngazi ya Halmashauri kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2025 zimewasilishwa na kujadiliwa.
Jumla ya Kamati 5 za kudumu za Halmashauri zimewasilisha taarifa zake ambapo Waheshimiwa Madiwani wamezipokea na kuzijadili.
Kamati zilizowasilisha taarifa ni pamoja na kamati ya Fedha Uongozi na Mipango, Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira, Kamati ya Elimu Afya na Maji, Kamati ya Kudhibiti UKIMWI na Kamati ya Maadili.
Akizungumza katika baraza hilo Mwenyekiti wa Mkutano huo ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe Silvester Kahesi amewapongeza madiwani na wataalam kwa namna ambavyo wamekuwa wakishirikiana katika vikao vya kamati hadi kufikia baraza.
" Ushirikiano hautakuja kama kuna upande utakuwa umejitenga, nitoe wito kwa madiwani na wataalam kuwa kitu kimoja ili kuleta ufanisi na kuijenga halmashauri kwa kuwa Sisi ni taswira ya Halmashauri hivyo kile tunachokifanya kika akisi matamanio ya wananchi” Amesema Mhe Kahesi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Ndg Karia Magaro Magaro amewasihi Waheshimiwa Madiwani kusimamia Sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji wa Halmashauri ili maamuzi yatakayokuwa yanachukuliwa yafanyike kwa hekima na busara ili kuendelea kulinda utulivu wa Halmashauri.
"Nitoe wito kwa Waheshimiwa Madiwani Kila mmoja kwenye kata yake anayoisimamia aijue miradi inayotekelezwa na kushirikiana na wataalam ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati kuweza kuwahudumia wananchi” Amesema Magaro
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilayani Geita Komredi Barnabas Mapande ametoa pongezi kwa Mkurugenzi Mtendaji kwa kusimamia fedha ambazo Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anazileta katika Halmashauri kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Tunaendelea Kumpongeza Mkurugenzi kwa kuzisimamia fedha zinazoletwa na Mhe Rais na ukusanyaji wa mapato. Tuendelee kuweka nguvu kulisukuma gurudumu kwa kuweka nguvu kwenye makusanyo ya mapato kwa kuendelea kushirikiana na Mkurugenzi na watendaji ili miradi ikamilike” Amesema Mapande.
Vilevile Komredi Mapande amesema Halmashauri ya Wilaya ya Geita ina maeneo mengi ya uchimbaji wa madini hivyo hakuna budi kuweka nguvu ya kukusanya mapato. “Kama Chama tutaendelea kuwa na ushirikiano kwa kuwa bega kwa bega na serikali ili kuleta tabasamu kwa wananchi" Ameongeza Komredi Mapande
Kwa upande wake Mhe Diwani kata ya Bukoli Mhe Faraj Seif kwa niaba ya Madiwani ametoa pongezi kwa Mkurugenzi Mtendaji kwa usimamizi mzuri wa Halmashauri katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo ndani ya Halmashauri ikiwepo na ukusanyaji wa mapato
"Sisi Madiwani tuna waahidi tutakuwa na utulivu katika Halmashauri yetu kuisaidia Serikali " Amesema Mhe Faraj Seif
Kwa upande mwingine Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Geita Ndg Munguatosha Macha ametoa rai kwa waheshimiwa madiwani kuendelea kutoa ushirikiano kwa halmashauri katika kusimamia na kukusanya mapato ili kuendelea kuongeza ajira kupitia mapato ya asilimia 10 yanayotolewa na Halmashauri.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa