Na Hendrick Msangi
BARAZA la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Geita Februari 13 na 14 katika kikao chake cha kawaida limepokea taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Serikali ngazi ya Kata na uwasilishaji wa taarifa za kamati ya fedha uongozi na mipango, kamati ya uchumi,ujenzi na mazingira, kamati ya elimu afya na maji pamoja na kamati ya kudhibiti Ukimwi kwa kipindi cha Octoba hadi Disemba 2023.
Jumla ya Kata 37 ziliwasilisha taarifa za utekelezaji wa shughuli za serikali katika maeneo yao ambapo Madiwani hao walijika kwenye changamoto mbalimbali zikiwemo za upungufu wa watumishi katika sekta ya elimu na afya, kuharibika kwa miundombinu ya barabara pamoja na ucheleweshwaji wa vifaa kwa ajili ya kukamilisha miradi inayotekelezwa na CSR kunakopelekea mafundi kukaa site mda mrefu.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mhe Charles Kazungu akiwa na Makamu mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe Hadija Said Joseph wakati wa Kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri.
Awali akifungua kikao hicho, Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mhe Charles Kazungu aliwataka madiwani hao kuzingatia kanuni za uendeshaji wa kikao hicho ili kufikia lengo la kikao hicho.
Akizungumza katika Baraza hilo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita ndugu Karia Rajabu Magaro aliwasihi Madiwani hao kuendelea kutoa ushirikiano kwa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita ili kuendelea kufuata taratibu zote na kuzizingatia kwa manufaa ya Halmashauri. “Mahali popote mnapo ona kuna uvujaji wa Mapato tufahamishane ili kuchukua hatua za ufuatiliaji kwa manufaa ya Halmashauri” alisema Magaro.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita ndugu Karia Rajabu Magaro akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani ambapo amewasihi waheshimiwa madiwani kuendelea kutoa ushirikiano ili Halmashauri hiyo iendelee kukusanya mapato katika vyanzo vyake
Aidha aliwasihi Madiwani hao kuendelea kutoa ushirikiano kufuatilia wazazi ambao hawajawapeleka watoto shule ili kuendelea kuinua kiwango cha ufaulu huku akitaja kiwango cha ufaulu kwa mitahani ya Kitaifa kwa kidato cha pili na cha nne kwa mwaka 2023 kuongezeka ambapo kwa kidato cha pili kiwango cha ufaulu kikiwa ni asilimia 83.47 kulinganisha na mwaka 2022 ambapo kiwango cha ufaulu kilikuwa asilimia 82.7 sawa na ongezeko la asilimia 0.77
Na kwa upande wa kidato cha nne kiwango cha ufaulu kimeongezeka kwa asilimia 9.14 ambapo mwaka 2022 ufaulu ulikuwa asilimia 77.80 kulinganisha na matokeo ya mwaka 2023 ambapo ufaulu umekuwa asilimia 86.81
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Geita ndugu Cornel L.B Magembe alizitaka Taasisi za RUWASA, TARURA na TANESCO kuhudhuria kwenye vikao vya kamati za Madiwani na Watumishi wa Halmashauri ili kuweza kuwa na taarifa zenye utoshelevu kuwafikia wananchi,
Akizungumzia swala la miradi viporo, Magembe alisema ni vema ikamilishwe kwa ajili ya kuwapelekea wananchi huduma “Tuweke nguvu ya ziada kukamilisha miradi ambayo ni viporo na kuacha kuanzisha miradi mipya ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya utekelezaji wa miradi ya CSR iliyopita” alisema Magembe.
Kuhusu upungufu wa walimu wa kike, Magembe alisema ipo haja ya kuhamisha walimu hao kwa shule ambazo wapo wengi na kuwapeleka kwenye shule zenye upungufu hivyo kuitaka halmashauri kuweka bajeti kwenye mapato yake ya ndani kwa ajili ya zoezi hilo ambapo ofisi ya Mkurugenzi ilisema itaendelea kuweka msawazo wa walimu wa kike ambapo jumla ya shule za msingi 18 hazina walimu wa kike na 14 za sekondari
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Geita Komredi Barnabas Mapande alilitaka baraza hilo kuhakikisha miradi viporo inakamilishwa kwa wakati ili kuwaondolea wananchi kero na kuepuka kuanzisha miradi mipya kwani wananchi wanahitaji miradi iliyokamilika ili kuendelea kuwa na Imani na serikali yao.”Tutumie fedha za CSR kukamilisha miradi yetu” alisema Mapande
Kufuatia upungufu wa walimu wa Kike Mapande alisema ipo haja ya mkoa wa Geita kuiomba Serikali kuongeza walimu wa kike kwani upungufu wa walimu hao unasabisha watoto wa kike kukosa msaada pale inapobidi.
Kuhusu swala la miundombinu ya barabara kuwa mibovu na kutokukamilika kwa wakati,Meneja wa TARURA Mhandisi Bahati Subeya alisema pamoja na changamoto ambazo zinajitokeza wakati wa utekelezaji wa miradi zikiwepo mvua zinazoendelea kunyesha, baadhi ya wananchi kuziba mifereji ya kutolea maji ya mvua pamoja na ufinyu wa bajeti ukilinganisha na mahitaji halisi ya matengenezo ya barabara ofisi ya TARURA itaweka kwenye mpango wa bajeti zijazo kulingana na ukomo wake kwa ajili ya utekelezaji kwa kuwa miundombinu mizuri ya barabara huinua uchumi wa halmashauri.
Kwa upande wa huduma za Maji safi na salama, Ofisi ya RUWASA ilisema ni vema Madiwani hao kuendelea kuzisimamia shule, Zahanati na vituo vya afya kulipa gharama za maji ili kuisaidia RUWASA kuendelea kuendesha miradi ikiwa ni pamoja kusaidia kulinda vifaa vinavyopelekwa kwenye miradi kwani kumekuwa na tabia ya wizi wa vifaa hivyo ili kuendelea kunuifaika na maji safi na salama.
Kuhusu Mradi wa Kimkakati wa Soko la Katoro, Madiwani hao waliazimia kupunguza bei ya pango kwenye soko hilo ili kuendelea kuvutia wananchi kwa ajili ya kufanya biashara katika soko hilo huku wakishauri Masoko ya dhahabu kuhamishiwa kwenye soko hilo ikiwa ni pamoja na kutengeneza miundombinu ya barabara inayoelekea kwenye soko hilo ili magari yaweze kufika eneo hilo ambapo Halmashauri itaongeza mapato.
Waheshimiwa madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita wakifuatilia kikao cha robo ya pili ambapo kwa pamoja waliazimia kushusha bei za pango kwa soko la kimkakati la Katoro ili kuendelea kuwavutia wafanya biashara kuwekeza katika soko hilo
Akihitimisha kikao hicho Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mhe Charles Kazungu aliwataka watendaji wa Halmashauri kuendelea kuweka bidii kwenye ukusanyaji wa mapato ili kutumia fedha za mapato ya ndani kuendelea kukamilisha miradi viporo. “Sitavumilia kuona mapato yanashuka, kwani fedha hizo ndio ndio zitatusaidia kutatua changamoto za wananchi” alisema Kazungu.
Aidha Mhe Kazungu aliwataka Waheshimiwa madiwani kushirikiana na wazazi kuhakikisha watoto ambao hawajaripoti kidato cha kwanza licha ya kufaulu waweze kuripoti haraka iwezekanavyo kwani gharama za elimu zipunguzwa na Serikali inayoongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku akisisitiza swala la lishe kuwa ni la lazima na sio la hiyari na kuwataka madiwani hao kuendelea kuhamasisha wazazi ili watoto wasipatwe na udumavu ambao unaweza kuepukika.
Kufuatia kikao chake hicho cha kujadili taarifa za utekelezaji wa shughuli za Serikali kwa kipindi cha Octoba hadi Disemba, Baraza la Madiwani limewafukuza kazi watumishi watatu kwa sababu za utoro kazini, huku watumishi wawili wakipewa onyo kali na mtumishi mmoja kutakiwa kufanya kazi yalipo makao makuu ya Halmashauri hiyo kwa kuendelea kuangaliwa mwenendo wake wa utekelezaji wa kazi.
Madiwani hao wameiomba Serikali sikivu ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kuendelea kuziunga mkono nguvu za Wananchi katika ujenzi wa Miradi mbalimbali inayotekelezwa kwenye maeneo ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita ili kusaidia kuinua ari ya wananchi ya kujitolea katika shughuli mbalimbali za maendeleo kwenye maeneo yao.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa