Na Hendrick Msangi
BARAZA LA MADIWANI Halmashauri ya Wilaya ya Geita Januari 19, 2024 limepitisha mpango na Bajeti kwa mwaka 2024/2025 katika kikao chake kilichiofanyika kwenye ukumbi wa mikutano uliopo Makao Makuu ya Halmashauri hiyo kata ya Nzera Wilayani Geita.
Wajumbe waa kikao maalumu Cha Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Geita kilichoketi Januari 19, 2024 kujadili na kupitisha mpango na bajeti kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita inapendekeza kukusanya na kutumia jumla ya shilingi 92,134,387,046.18 ampapo shilingi 17,668,215,000.00 ni fedha za ruzuku zitakazotumika kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo, shilingi 1,556,073,000.00 ni ruzuku zitakazotumika kwa matumizi ya kawaida (OC) Shilingi 64,942,698,078.00 zitatumika kulipa mishahara ya watumishi Shilingi 6,974,747,368.18 ni makusanyo ya ndani ambayo Halmashauri hiyo inatarajia kukusanya kupitia vyanzo mbalimbali vya mapato ukiondoa mapato fungwa.
Akizungumza Katika Baraza hilo Kaimu Mkuregenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Bi Sarah Yohana amesema bajeti hiyo imezingatia Miongozo kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, dira na dhamira ya Halmashauri, Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya 2020-2025 pamoja na sheria ya bajeti na kanuni zake huku akivitaja vipaumbele vikubwa ambavyo Halmashauri imeweka katika bajeti hiyo ni pamoja na kuongeza mapato kwa kusimamia na kudhibiti ukusanyaji wa mapato, kuboresha miundombinu ya afya na elimu ambazo ni sekta za kijamii huku swala la lishe likipewa kipaumbele katika bajeti hiyo na kwa upande wa wadau wa maendeleo Halmashauri itashirikiana na GGML, BUCKREEF, NELICO, PLAN INTERNATIONAL, MDH, KIVULINI, SONGAMBELE, ICAP,CODERT na SEDIT.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Bi Sarah Yohana akifuatili kwa makini kikao cha Baraza la Madiwani kilichoketi kujadili na kupitisha mpango na bajeti kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Geita Bi Lucy Beda alisema ili kuweza kuifikia bajeti hiyo ni vema Halmashauri kuweka mipango mizuri ya kusimamia na kudhibiti ukusanyaji wa mapato katika vyanzo vyake ambapo kwa kufanya hivyo bajeti hivyo utekelezaji wa bajeti hiyo utafanyika kwa ufanisi.
Katika Baraza hilo Katibu wa Chama cha Mapinduzi Wilayani Geita Komredi Michael Msuya aliwapongeza madiwani kwa kupitisha bajeti hiyo kwani imezingatia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi na kuwataka madiwani hao kuwa na usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo kuhakikisha dhamira ya Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwaletea wananchi maendeleo inatimia kupitia bajeti hiyo.
Akizungumza katika baraza hilo la Madiwani, Mkuu wa Wilaya ya Geita ndugu Cornel Magembe alisema anaimani kubwa na Halmashauri katika kutekeleza bajeti iliyopangwa kwani miradi mingi imekuwa ikitekelezwa vizuri na kwa viwango sahihi huku akisema bajeti hiyo itaenda kujibu matarajio ya wananchi.
Aidha Magembe amelipongeza baraza hilo kwa kuendelea kutekeleza miradi mingi kwa ufanisi ambayo serikali inatoa fedha na kuwataka Madiwani hao kuendelea kushikamana kwa umoja kuwatumikia wananchi.” Tunapokuwa tumeweka mipango yetu ni katika kumsaidia Mhe Rais kuwaletea maendeleo wananchi kwa fedha ambazo tumepanga kukusanya na ambazo serikali kuu inatoa kwa ajili ya utekelezaji wa mpango na bajeti tuliyoipanga” alisema Magembe.
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe Cornel Magembe akihutubia kikao Maalumu Cha Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Geita kilichoketi Januari 19, 2024 kujadili na kupitisha mpango na bajeti kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Naye Diwani wa viti maalum katoka Kata ya Ludete Mhe Maimuna Buriro (Mama Mingisi) ameipongeza bajeti hiyo na kusema itapelekea kutekeleza miradi waliyoipitisha kwani Halmashauri itaenda kukusanya na kuvuka lengo la ukusanyaji walilojiwekea.
Akifunga kikao cha baraza hilo, Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Geita Mhe Charles Kazungu aliwashukuru wajumbe wote na kusema maelekezo yote yaliyotolewa na viongozi yatafanyiwa kazi ili kuifikia bajeti hiyo na kusisitiza kuwa baraza la madiwani litaendelea kutoa ushirikiano na kuweka bidii katika ukusanyaji wa mapato kwenye kata zote 37 za Halmashauiri ya Wilaya ya Geita ili kufikia lengo la bajeti hiyo iliyopitishwa kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa