Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Agosti 7, 2024 limeendelea na kikao chake cha kawaida kwa siku ya pili ambapo kamati za Baraza hilo zimewasilisha taarifa za utekelezaji wa shughuli za serikali kwa robo ya nne April hadi Juni 2024.
Kamati zilizowasilisha taarifa ni pamoja na Kamati ya Fedha, uongozi na Mipango, Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira, Kamati ya Elimu, Afya na Maji, Kamati ya Kudhibiti UKIMWI na Kamati ya Maadili.
"Tusimamie mashine za kukusanya mapato ya serikali (Posi) kwa kuzingatia matumizi ya posi na tujiwekee mikakati mapema ili makusanyo yetu yaweze kwenda vizuri"Hashim Abdallah Komba Mkuu wa Wilaya ya Geita
Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni diwani wa kata ya Butobela Mhe. Charles Kazungu amewapongeza madiwani wa Kata zote 37 kwa ukusanyaji mzuri wa mapato Kwa mwaka wa fedha 2023/2024 uliopelekea Halmashauri kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 7.3 sawa na asilimia 107.88
Tuendelee kusimamia kukusanya mapato yetu kwa haki kwa kufuata sheria , kanuni na taratibu bila kumuumiza mfanyabiashara na mwananchi yeyote .Ndg Karia Magaro Mkurugenzi Mtendaji
Aidha Mhe. Kazungu amewasisitiza madiwani wote kufanya kazi kwa bidii zaidi kwa mwaka mpya wa fedha 2024/2025 ili kuweza kukusanya mapato ya kutosha katika maeneo yao. "Niwaombe sana kasi ile tuliyokuwa nayo 2023/2024 tuende nayo 2024/2025 tena kwa kasi ya 5G". Amesisitiza Mhe. Kazungu katika kikao cha baraza hilo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Abdallah Komba amewasisitiza madiwani wa Kata zote kushirikiana vema na vyombo vya usalama ili kuweza kulinda hali ya ulinzi na usalama katika maeneo yao kutokana na kuwepo kwa matukio mengi ya kihalifu kama vile uporaji, ukabaji, pamoja na vitendo vya kikatili kwa watu wenye ulemavu wa ngozi.
"Nawapongeza kwa ukusanyaji wa mapato na miradi inayoendelea kufanyika. Pia Mkurugenzi kwa namna ambavyo unawaunganisha watumishi kukaa pamoja na kuendelea kutenda haki kunakopelekeawatumishi kufanya kazi na chama cha mapinduzi (CCM) kitaendelea kuwa pamoja na serikali" Komredi Barnabas Mapande Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Geita
Sambamba na hayo Mhe. Komba amelipongeza baraza la madiwani kwa kazi nzuri wanayoifanya ikiwa ni pamoja na ukusanyaji mkubwa wa mapato yanayowawezesha kuendesha shughuli mbalimbali za kimaendeleo na ushirikiano walio nao katika kuisaidia Halmashauri kufikia malengo yake.
Naye Mbunge wa Jimbo la Busanda Mhandisi Magesa ameiomba kamati ya ulinzi na usalama kuendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika Kata ya Butundwe kwa kushughulikia kikamilifu suala la wizi na kuuliwa kwa ngo'mbe pamoja na viboko ambao wamekua tishio katika ukanda huo kutokana na kusababisha vifo kwa baadhi ya wakazi wa eneo hilo."Niiombe kamati ya ulinzi na usalama iwasaidie Wananchi wa kata ya Butundwe kupambana na viboko hao kwani wamekua tishio kutokana na matukio mengi yanayoendelea kutokea kila leo". Amesema Mhe. Magesa
"Niwaombe kasi ile ile ya mwaka 2023/2024 tuendelee nayo kwa kasi zaidi kwa mwaka 2024/2025 tujifunge mkanda ili tuendelee kukusanya zaidi." Mhe Charles Kazungu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Vilevile Baraza la madiwani katika kikao hicho limeazimia kuwarejesha kazini Ndg Mick Chotta aliyekuwa mtumishi kitengo cha sheria pamoja na Ndg Abdallah Mkumbo aliyekuwa Afisa utumishi daraja la kwanza ambao walisimamishwa kazi Kutokana na mashauri ya kinidhamu. Hatua hiyo imefikiwa kutokana na uchunguzi uliofanyika kupitia kamati mbalimbali ikiwemo kamati za madiwani na kubaini kukosekana kwa hatia kwa watumishi hao.
Katika baraza hilo, Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Geita Ndg Karia Magaro amewaomba Waheshimiwa madiwani kuendelea kushirikiana katika kusimamia miradi ya maendeleo inayoendelea katika maeneo yao kwa ufanisi na ubora uliokusudiwa na kuwahikikishia kuendelea kuwa bega kwa bega na timu ya menejimenti ya halmashauri
Aidha Ndg Magaro ameendelea kuishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuleta fedha nyingi za miradi ambayo imepunguza adha kwa wananchi na kuwataka madiwani kuendelea kujitoa ili malengo ya Halmashauri yaendelee kutimia kwa mwaka 2024/2025.
kikao cha baraza la madiwani Agosti 7 kujadili taarifa za maendeleo ambapo jumla ya kamati 5 ziliwasilisha taarifa za utekelezaji wa shughuli za maendeleo.
Baraza hilo limehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa chama na serikali akiwepo kamati ya Ulinzi na Usalama ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe Hashim Komba, Katibu tawala wilaya Bi Lucy Beda, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Geita Cde Barnabas Mapande, Waheshimiwa wabunge wa Jimbo la Geita vijijini Mhe Joseph Kasheku Musukuma, Mbunge wa Jimbo la Busanda Mandisi Tumaini Magesa, wakuu wa Idara na Vitengo, kikundi cha vijana wajasiriamali Halmashauri ya Geita na wakuu wa taasisi za umma,
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa