Na: Nyamizi Elias
BARAZA la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Geita likiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Charles Kazungu Agosti 29, 2024 limefanya kikao chake maalum cha uwasilishaji wa hesabu za mwisho kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Akiwasilisha taarifa ya ukamilishwaji wa hesabu hizo Mweka hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Bi Eveline Richard amesema, kazi ya uwasilishwaji wa hesabu ya mwaka 2023/2024 ilianza mapema Julai 2024 na kukamilika rasmi Agosti 25, 2024.
Waheshimiwa Madiwani wakiwa katika Kikao cha Baraza Maalum la ufungaji wa hesabu za Sererikali kwa upande wa Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Aidha Bi Eveline ameeleza kuwa hesabu za fedha kwa mwaka wa fedha 2023/2024 zimegawanyika katika maeneo tofauti tofauti ambayo ni taarifa mbalimbali za Halmashauri, maelezo ya jumla ya fedha kwa mwaka wa fedha 2023/2024 pamoja na taarifa za hesabu kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Mweka Hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Bi Eveline Richard akiwasilisha taarifa ya ufungaji wa hesabu kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Vilevile Bi Eveline katika uwasilishaji wake amechanganua zaidi mgawanyiko wa fedha kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kwa kuonesha fedha zilizokuwepo kuishia Juni 30, 2024 ni kiasi cha shilingi Bilioni 9.5, wadaiwa wa Halmashauri shilingi Bilioni 8.17, Uwekezaji mfuko wa Serikali za mitaa ni shilingi 87.3, Mali za Halmashauri zisizohamishika ni shilingi Bilioni 90.49, wadaiwa wa Halmashauri ni shilingi Bilioni 1.76 pamoja na kuonesha mapato na matumizi ya Halmashauri ambapo mapato ni jumla ya kiasi cha shilingi Bilioni 85.8 huku matumizi ikiwa ni shilingi Bilioni 87.5.
Katibu Tawala wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Bi Lucy Beda akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Ndg Karia Magaro wakati wa Kikao cha Baraza la Madiwani la uwasilishaji wa taarifa ya Ufungaji wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ambapo Mkurugenzi Mtendaji amelipongeza baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa ukusanyaji mzuri wa mapato uliochochea kukamilisha kwa wakati uandaaji wa taarifa ya hesabu ya mwaka wa fedha 2023/2024.
Mbali na hayo Bi Eveline pia ameeleza dhima na madhumuni ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ikiwa ni pamoja na kuendeleza ubora wa elimu ya Msingi na Sekondari, ubora wa huduma za afya, kubaini vyanzo vipya vya mapato pamoja na kuboresha ukusanyaji na usimamizi wa matumizi.
Katika kuwasilisha taarifa hiyo, Mweka hazina huyo amewashukuru viongozi na wadau wote wa ukusanyaji wa mapato kwa ushirikiano waliouonesha katika kuhakikisha wanakamilisha uwasilishwaji wa taarifa ya hesabu ya mwaka wa fedha 2023/2024.
Kwa upande wake Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM ) Wilaya ya Geita Komredi Gabriel Masunga ameupongeza uongozi mzima wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa uchapakazi bora katika ukusanyaji wa mapato na kuwaasa wananchi kuendelea kuwapa ushirikiano viongozi wao ili kuweza kukusanya mapato zaidi kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Akizungumza Katika Baraza hilo Katibu tawala wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Bi Lucy Beda amelipongeza Baraza la Madiwani, Mkurugenzi Mtendaji na watendaji kwa uchapaji kazi mzuri wenye ufanisi unaongeza mapato katika Halmashauri.
Waheshimiwa Madiwani wakiwa katika Kikao cha Baraza Maalum la ufungaji wa hesabu za Sererikali kwa upande wa Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Pamoja na hayo , Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Ndg Karia Magaro ameishukuru Serikakali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe Dkt Samia Suluh Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za maendeleo kwa kutoa fedha kwa watumishi pamoja na kutoa fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo.
Akihitimisha kikao hicho Mwenyekiti wa baraza la madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mhe Charles Kazungu amewasihi Waheshimiwa Madiwani kuendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wakusanyaji wa mapato ili kuweza kutimiza malengo waliyojiwekea ya kukusanya mapato zaidi kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa