BARAZA la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Geita Februari 7, 2025 katika Mkutano wake Maalum uliofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri-Nzera limepitisha rasimu ya Bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kiasi cha Shilingi Bilioni 93.5
Awali akiwasilisha mapendekezo ya mpango na bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Afisa Mipango wa Halmashauri Bi Sarah Yohana amesema Halmashauri ya Wilaya ya Geita inapendekeza kukusanya na kutumia jumla ya Tsh Bilioni 93.5 ambapo kiasi cha Tsh Bilioni 16.5 ni fedha za ruzuku zitakazotumika kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo.
Aidha Bi Sarah ameongeza kwa kusema katika bajeti hiyo kiasi cha Tsh Bilioni 1.5 ni ruzuku zitakazotumika kwa matumizi ya kawaida, Tsh Bilioni 63.5 zitatumika kwa ajili ya kulipa mishahara ya watumishi huku kiasi cha Tsh Bilioni 11.9 ni mapato ya ndani.
Afisa Mipango wa Halmashauri Bi Sarah Yohana akiwasilisha Rasimu ya Bajeti kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji katika mkutano maalum wa Baraza la madiwani wa kujadili mapendekezo ya mpango na Bajeti kwa Mwaka 2025/2026
Akizungumza katika Baraza hilo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mhe Charles Kazungu amelipongeza Baraza la Madiwani kwa kupitisha bajeti hiyo ya kiasi cha Shilingi Bilioni 93.5
“Niwapongeze watumishi wetu chini ya Mkurugenzi makini bingwa kabisa Karia Rajabu Magaro kwa uandaaji mzuri wa bajeti yetu ya 2025/26 mmeandaa vizuri” amesema Mhe Kazungu.
Mhe Kazungu ametoa rai kwa watumishi na waheshimiwa madiwani kuendelea kuwa na ushirikiano ili kufikia lengo la bajeti hiyo. “Tuendelee kukaza buti ili tufikie malengo ya makusanyo na kuvuka asilimia za makusanyo, tuendelee kushikamana katika bajeti hii tunayoendelea nayo ili tuvuke lengo moto tuliokuwa nao usizimike” Ameongeza Mhe Kazungu.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mhe. Charles Kazungu akizungumza katika mkutano maalum wa Baraza la Madiwani wa kujadili mapendekezo ya Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/2026
Vilevile Mhe Kazungu amesema lengo la Bajeti hiyo ni kwenda kuwatumikia wananchi kwa kuwa jiografia ya Halmashuri ya Wilaya ya Geita ni kubwa na Halmashauri inayo wajibu wa kupeleka kwa wananchi kwa kuwa bajeti hiyo imezingatia kila kipaumbele katika utekelezaji.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Geita Ndg Karia Rajab Magaro amelipongeza baraza hilo kwa namna ambavyo limeshirikiana na watumishi katika kufanya kazi na kupeleka makusanyo kutoka Bilioni 5 hadi kufika Bilioni 8 na kwenda kukusanya bilioni 11 kwa mwaka wa fedha 2025/26.
“Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anasisitiza tukusanye mapato ili Halmashauri ziweze kujitegemea hivyo niwaombe waheshimiwa madiwani kuendelea kushirikiana ili bajeti ziendelee kukua na kuwasaidia wananchi” Amesema Magaro.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Nag. Karia Magaro akizungumza katika mkutano maalum wa baraza la Madiwani wa kujadili mapendekezo ya mpango na bajeti kwa mwaka 2025/2026
Naye Katibu Tawala Wilaya ya Geita Bi Lucy Beda katika Baraza hilo ameipongeza Halmashauri kwa kuweza kufika asilimia 58.3 ya makusanyo katika bajeti kwa mwaka wa fedha 2024/25 na kutoa wito kwa madiwani kuendelea kuisimamia Halmashauri ili malengo ya utekelezaji yaweze kufikiwa. “Naamini bajeti hii iliyowekwa itakwenda kuwafikia wananchi” Amesema Bi Lucy Beda.
Aidha Katibu Tawala amemtaka Mkurugenzi Mtendaji na Watumishi wa Halmashauri kuendela kuibua vyanzo vingine vya mapato ili kuendelea kuwa na mapato makubwa. “Tunavyo vyanzo mbalimbali vya mapato tukavisimamie na kuibua vyanzo vingine ili kuendelea kuwa na mapato makubwa zaidi na kusimamia tulivyo navyo vema.” Ameongeza Bi Lucy Beda.
Pamoja na hayo Katibu Tawala ametoa wito kwa madiwani kuipa kipaumbele Kata ya Izumacheli iliyo kisiwani kufuatia kuwa na miundombinu duni ya barabara na kuielekeza taasisi ya wakala wa barabara vijijini na mijini (TARURA) kuipa kipaumbele kata hiyo katika kuimarisha miundombinu ya barabara.
Waheshimiwa madiwani wakipitia rasimu ya bajeti katika mkutano maalum wa baraza la Madiwani wa kujadili mapendekezo ya mpango na bajeti kwa mwaka 2025/2026
Baraza hilo limeidhinisha jumla ya kiasi cha Tsh Bilionin 110.4 ambapo bajeti ya Halmashauri ni Bilioni 93.5, TARURA Bilioni 5.1 na RUWASA ni Bilioni 11.7 ambazo zitatumika katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa