Na Michael Kashinde
Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Geita likiwa katika mkutano maalumu wa kujadili mpango na bajeti Januari 24, 2023 limejadili na kupitisha bajeti ya kiasi cha shilingi bilioni 87.2 ikiwa ni makusanyo na matumizi kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Akiwasilisha mapendekezo ya mpango na bajeti katika mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Nzera Afisa Mipango Halmashauri ya Wilaya ya Geita Bw. Walter Anthony amefafanua kuwa kiasi cha shilingi bilioni 15.08 ni fedha za ruzuku zitakazotumika kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo.
Bw. Walter ameeleza kuwa kiasi cha shilingi bilioni 2.5 ni ruzuku zitakazotumika kwa matumizi ya kawaida (OC), shilingi bilioni 62.5 zitatumika kulipa mishahara ya watumishi, shilingi bilioni 6.3 ni makusanyo ya ndani ukiondoa mapato fungwa, na kiasi cha shilingi milioni 669.9 ni mapato mengine kama CHF, NHIF, na tozo za minara shuleni.
Miongoni mwa vipaumbele vilivyozingatiwa katika mpango na bajeti hiyo ni pamoja na kusimamia na kudhibiti ukusanyaji wa mapato kwa kununua POS mpya 40 na gari kwa ajili ya usimamizi na ufuatiliaji, sambamba na kuongeza miundo mbinu katika Sekta ya Elimu ambapo Halmashauri inatarajia kujenga shule tatu mpya na kukamilisha vyumba vya madarasa 70 kwa shule za msingi.
Aidha vipaumbele vingine ni pamoja na kuboresha minada ya Katoro, Bugalama, Kamena na Kakubilo pamoja na stendi za mabasi Rwamgasa, Nkome, Katoro na Nyarugusu ili kuongeza vyanzo vya mapato, sambamba na mapambano dhidi ya UKIMWI, Rushwa, uharibifu wa mazingira na unyanyasaji wa kijinsia (MTAKUWA).
Akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Geita Bw. Fredy Mhagama amewataka Waheshimiwa Madiwani ambao ni Wenyeviti wa Kamati za maendeleo za Kata kuendelea kuhamasisha ulinzi shirikishi katika maeneo yao ili kudhibiti vitendo vya wizi wa mifugo ambavyo vinafanyika katika baadhi ya maeneo.
Aidha Bw. Mhagama ametumia nafasi hiyo pia kuwataka viongozi kuanzia ngazi za vijiji kujenga utaratibu wa kuwasomea wananchi taarifa za mapato na matumizi katika maeneo yao ili kuepuka kuichonganisha Serikali na Wananchi huku akiwakumbusha Watendaji wa Kata kuacha kukaa na fedha za Serikali badala yake waziwasilishe Benki kama miongozo inavyowataka.
Akihtimisha kikao hicho cha siku moja Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mhe. Charles Kazungu ametoa wito kwa waheshimiwa madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita kuhakikisha wanahamasisha jamii katika maeneo yao kuwapeleka wanafunzi mashuleni ili kufikia jumatatu ya Januari 30, 2023 watoto wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wawe wameripoti kwenye shule walizopangiwa kuendelea na masomo.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita inatarajia kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo GGML, BUCKREEF, NELICO, PLAN INTERNATINAL, MDH, KIVULINI, SONGAMBELE, ICAP, CODERT,na SEDIT katika kuandaa na kutekeleza mpango na bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 uliopitishwa na baraza la madiwani wenye jumla ya kiasi cha shilingi 87,224,875,671.00
PICHA ZAIDI
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa