Na. Michael Kashinde
Baraza la madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Geita Oktoba 7, 2022 limemshukuru Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Halmashauri ya Wilaya Geita kiasi cha Tsh. 5,340,000,000 (Bilioni 5 na Milioni 340) kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 267 vya madarasa katika shule za Sekondari 39 kwa ajili ya kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2023.
Akitoa neno la shukrani katika mkutano maalumu wa baraza la Madiwani kwa niaba ya wajumbe wa baraza hilo, uongozi wa Chama Cha Mapinduzi na Serikali Wilaya ya Geita Mhe. Elisha Lupuga mwenyekiti wa kamati ya fedha, uchumi na mipango na diwani wa kata ya Bugulula, amesema kuwa viongozi, watumishi, na wananchi wa Halmashauri ya Wilaya Geita wanamshukuru sana Mhe. Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa nia yake njema ya kuwasaidia wanafunzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
“Mhe.Mwenyekiti tunaomba tuungane kwa pamoja wajumbe wote wa baraza hili ukiwemo Mhe. Mkuu wa Wilaya na viongozi wote wa Chama kuendelea kumshukuru Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutupatia kiasi cha Tsh. 5,340,000,000."
Ameendelea kusema kuwa "hakika watumishi, viongozi na wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita wanamshukuru sana kutokana na nia yake njema kwa watoto wa Halmashauri yetu kwa kuwapatia vyumba 267 vya madarasa na ni matumaini yetu kuwa watoto wote watakaochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2023 watapata vyumba vya madarasa vyenye ubora na mandhari nzuri kwa niaba ya Halmashauri tunamshukuru sana Mhe. Rais.” amesema Mhe. Lupuga.
Kwa upande wake Mwl. Hossana Mussa Nshullo Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari Halmashauri ya Wilaya ya Geita akieleza mikakati ya utekelezaji wa ujenzi wa madarasa hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, amesema kuwa timu ya Menejimenti imeazimia kutekeleza miradi hiyo kupitia Force Account ambapo pia zitaundwa kamati tano kwa ajili ya ufuatiliaji wa karibu wa miradi hiyo.
Mwl. Nshullo amebainisha kamati hizo kuwa ni pamoja na kamati ya usimamizi na ufuatiliaji ngazi ya Wilaya na Halmashauri, kamati ya usimamizi na ufuatiliaji ngazi ya Kata, kamati ya ujenzi ngazi ya shule, kamati ya manunuzi ngazi ya shule na Halmashauri na kamati ya Mapokezi ngazi ya shule na Halmashauri.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuelekea miradi hiyo ikiwa ni pamoja na maandalizi ya manunuzi ya vifaa vya viwandani ambayo yanaendelea kupitia kitengo cha manunuzi cha Halmashauri.
Aidha Halmashauri inafanya tathmini ya maboma yote yaliyopo kwenye maeneo ya shule Mama na shule mpya zinazopendekezwa ili kujua thamani ya fedha iliyotumika huku mawasiliano na watendaji wa Kata yakiendelea ili kuwaagiza kuwasilisha Mihtasari ya mapendekezo ya maeneo ya kujenga shule mpya za Sekondari.
Miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa na timu ya menejimenti ni pamoja na kuwahamasisha wananchi walio kwenye maeneo ambayo shule mpya zitajengwa, kujitolea kujenga miundombinu mingine kama vile vyoo na huduma zingine zinazohitajika katika mazingira ya shule, kwa kuwa fedha zilizotolewa zimeelekezwa kujenga madarasa na samani peke yake.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Wilson Shimo akizungumza katika mkutano huo, amewataka wajumbe kuhakikisha wanaisaidia jamii hasa watoto kupata lishe bora ambayo ina mchango katika maendeleo ya wanafunzi kitaaluma huku akilitaja suala la lishe duni kuwa kikwazo kikubwa cha matokeo mazuri kwa wanafunzi hasa wanapokaa muda mwingi bila kupata chakula wakiwa shuleni.
Aidha amewataka viongozi hao kuhakikisha wanatenga bajeti za chakula mashuleni huku akitoa wito kwa viongozi hao na walimu kwa ujumla kuongeza bidii ili kuwasaidia wanafunzi hao kufaulu vizuri huku akikemea tabia za baadhi ya wazazi wanaowalaghai watoto wao hasa wa kike wafanye vibaya katika mitihani ili wasiendelee na shule ambapo wakati mwingine huwaozesha.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Geita Ndg. Barnabas Mapande ametumia nafasi hiyo kumpongeza Mkurugenzi Mtendaji Adv. John Wanga na timu ya menejiment Halmashauri ya Wilaya Geita kwa kazi nzuri wanazozifanya huku akitoa wito wa kusimamia vizuri ujenzi wa miradi hiyo ya madarasa ili thamani na ubora wake uonekane kama ilivyo dhamira ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan.
Mapande ametumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wajumbe hao wanapozungumza na wananchi kuyasema wazi maendeleo yanayofanywa na Serikali kwa wananchi wake ili wananchi wajue, huku akishukuru kwa kuchaguliwa tena kuwa mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Geita.
Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita unaamini kuwa watoto wote watakaochaguliwa kujiunga na Kidato cha kwanza mwaka 2023 watapata vyumba vya madarasa vyenye ubora na mandhari nzuri, huku ukimuahidi Mhe. Rais pamoja na Serikali ya Mkoa na Wilaya kuwa, kazi hiyo ya ujenzi wa madarasa itafanyika kwa weledi, uadilifu na uwajibikaji wa hali ya juu.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa