Nzera-Geita
Mkutano wa Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Geita umeendelea Aprili 30,2025 katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri Nzera baada ya tarehe 29,2025 kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa shughuli za maendeleo ngazi ya kata.
Akizungumza katika Baraza Hilo Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Geita Ndg Karia Rajab Magaro ametoa pongezi kwa Waheshimiwa Madiwani kwa kusimamia jukumu la ukusanyaji wa mapato.
"Waheshimiwa Madiwani mmekuwa bega kwa bega na Menejimenti katika kushauri na kusisitiza ukusanyaji wa mapato ambapo hadi Machi 2025 Halmashauri imekusanya jumla ya Shilingi Bilioni 7.3 sawa na asilimia 88.26 ya mapato yanayotarajiwa kukusanywa kwa mwaka." Amesema Ndg. Magaro.
Aidha Mkurugenzi Mtendaji amesema Halmashauri imepanga kusimamia na kutekeleza miradi yenye thamani ya shilingi Bilioni 17.2 kutokana na mapato ya ndani , wahisani na Serikali kuu.
"Jumla ya Shilingi Bilioni 14.8 zimepokelewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kutoka Serikali kuu na wadau na Bilioni 3.1 kutoka mapato ya ndani."
Pamoja na hayo, Mkurugenzi Mtendaji ametoa rai kwa Waheshimiwa Madiwani kuendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ili kupata thamani ya fedha.
"Niendelee kuomba Ushirikiano kwa Madiwani kujitoa ili kukamilisha na kuvuka malengo kwa mpango wa 2024/2025." Amesema Ndg. Magari.
Aidha Ndg Magaro katika Mkutano huo wa Baraza la Madiwani Robo ya tatu, ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita inayo ongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutoa fedha nyingi za miradi ya Maendeleo hali iliyopelekea kupunguza adha kwa wananchi.
Vilevile Ndg Magaro amewashukuru Waheshimiwa Wabunge, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya kwa Ushirikiano mzuri ambao wamekuwa wakiutoa ili Halmashauri iendelee kufanya vizuri katika nyanja zote.
Katika Baraza hilo Waheshimiwa Madiwani wameipongeza ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji kwa kupata Hati safi kutoka kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
"Tuipongeze ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji kwa kuipa Halmashauri Hati safi ya Hoja za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amesema Mhe Hadija Said Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri.
Akihitimisha Kikao hicho cha Baraza Makamu Mwenyekiti Mhe Hadija Said amewashukuru Waheshimiwa Madiwani na Wataalam kwa namna walivyoshiriki Mkutano huo wa Baraza na kuwataka kuendelea kusimamia shughuli za maendeleo ikiwa ni pamoja na kufanya mikutano na wananchi katika maeneo yao.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa