Wahenga walinena mtoto ni Baraka, kauli hiyo imejidhihilisha tarehe 16 june 2019 kwenye maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika ambapo Serikali inatarajia kuanza ujenzi wa hospitali nyingine ya Wilaya katika mji mdogo wa Katoro uliopo Halmashauri ya wilaya ya Geita.
Hayo yameelezwa na Mgeni rasmi kwenye siku hiyo ambaye ni Waziri wa Afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto Ummy Mwalimu alipokuwa anajibu risala za viongozi mbalimbali akiwemo mkuu wa Mkoa Geita Mhandisi Robert Gabriel, amesema Kutokana na idadi kubwa ya watu, hospitali pekee iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Nzera haitokidhi hitaji.
Waziri Ummy amesema kuwa Serikali kupitia Wizara yake itatoa shilingi milioni 500 ili hospitali ianze kujengwa kwa haraka lakini pia amempongeza Mkuu wa mkoa wa Geita kwa kuahidi kutoa shilingi milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo.
Kutokana na kanda ya ziwa kuwa na idadi ya watu takribani milioni 13.4 Waziri amesema haiwezi kuwa na hospitali 1 ya kanda (Bugando), hivyo Serikali imeamua kujenga hospitali nyingine ya rufaa ya kanda mkoani Geita ili kupunguza haja ya wagonjwa kwenda Bugando.
Amesema Serikali inampango wa kuifanya hospitali hiyo itakayojengwa Geita kuwa ndio kituo cha utalii wa matibabu katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania pia italenga kuwavutia Nchi za jirani kama Congo, Rwanda na Burundi kuja kupata matibabu hospitalini hapo.
Hata hivyo Katika kuhakikisha watoto wanalindwa na kupata haki zao za msingi amesema kuwa Serikali imechukua hatua mbalimbali kukabiliana na changamoto zinazowakabili watoto Nchini, pamoja na kuridhia mikataba ya kimataifa na kanda kuhusu haki na ustawi wa watoto,Serikali imeandaa mipango na mikakati mabalimbali inayolenga kuwalinda na kuwaendeleza watoto katika Nyanja zote.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa Geita Mhandisi Robert Gabriel amesisitiza kila mzazi kuhakikisha mtoto anapata mahitaji muhimu kama Elimu na afya bora pamoja na kulindwa, pia kuachana na dhana ya kusema mtoto wa kiume ni bora zaidi ya wakike kwani nyakati hizi viongozi mbalimbali Duniani ni wanawake na wanafanya vizuri.
Aidha mkuu wa mkoa alimuahidi mgeni rasmi kuwa mwisho wa mwaka huu anatarajia kukabidhi zahanati 100 zinazojengwa katika kila kijiji ambazo kwa sasa ujenzi wa maboma umefikia takribani asilimia 96.
Ujumbe wa maadhimisho ya siku ya motto wa Afrika kwa mwaka 2019, ‘Mtoto ni Msingi wa Taifa Endelevu, Tumtunze, Tumlinde, na kumuendeleza’, ambapo waziri Ummy alizindua kampeni ya kimataifa ya usawa kwa motto wa kike(Girls Get Equal) iliyoandaliwa na shirika la Plan International.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa